NAIBU WAZIRI TAMISEMI APONGEZA MATUMIZI YA MAGARI YA UMEME KATIKA KUHIFADHI MAZINGIRA.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Jafar Seif, ametembelea banda la Wizara ya Nishati katika maonesho ya wiki ya Mazingira yanayoendelea kwenye Viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC) jijini Dodoma, ambapo amejionea teknolojia mbalimbali za nishati safi zinazolenga kuimarisha maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira nchini.
Akiwa katika maonesho hayo, Dkt. Seif ameweza kutembelea banda la Wizara ya Nishati ambapo amejionea gari aina ya Nissan Leaf linalotumia umeme na kupata maelezo kuhusu matumizi ya gari hilo linalotumika kuhamasisha wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi na teknolojia rafiki kwa mazingira.
Akizungumza katika banda hilo, Dkt. Seif amesema matumizi ya magari ya umeme ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo inachangia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa itokanayo na matumizi ya mafuta ya petroli na dizeli huku ikiunga mkono ajenda ya Taifa ya matumizi ya nishati safi.
“Magari ya umeme ni sehemu ya teknolojia za kisasa zinazosaidia kulinda mazingira na kuboresha ubora wa maisha ya wananchi hivyo ni muhimu kuendelea kuhamasisha matumizi yake ili Tanzania iende sambamba na mwelekeo wa dunia wa matumizi ya nishati safi,” amesisitiza Dkt. Seif.
Kwa upande wake, Mtaalamu kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Eneza Nyika, amesema kuwa UNDP kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati tumeendelea kuhamasisha matumizi ya magari ya umeme kutokana na manufaa yake ya kiuchumi na kimazingira.
Amefafanua kuwa magari hayo hayana kelele kabisa hayatoi moshi unaochafua mazingira,na hutumia umeme ambao ni wa gharama ndogo zaidi ikilinganishwa na mafuta ya kawaida.
Bw. Nyika ameongeza kuwa kuongezeka kwa matumizi ya magari ya umeme kutasaidia kuchochea uwekezaji katika miundombinu ya nishati safi, kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na kupunguza utegemezi wa mafuta.
Dkt. Seif ameipongeza Wizara ya Nishati pamoja na washirika wake wa maendeleo kwa kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya teknolojia za nishati safi. Amesema juhudi hizo zina mchango mkubwa katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na kuharakisha utekelezaji wa mikakati ya Taifa ya maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira.
Maonesho hayo yalianza tarehe 1 June 2026 yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 5 June 2026 katika kipindi hicho wananchi wanaendelea kutembelea mabanda mbalimbali ili kupata elimu na kujifunza kuhusu uhifadhi wa mazingira, matumizi ya nishati safi na teknolojia rafiki kwa mazingira.