NDEJEMBI ATOA MAAGIZO KWA PBPA RATIBA YA USHUSHAJI MAFUTA.
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ameutaka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuhakikisha maghala yote makubwa ya usambazaji wa mafuta yanapata bidhaa hiyo kwa wakati, ili kuimarisha upatikanaji wake nchini.
Akizungumza Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao na viongozi wa PBPA, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na kampuni ya Tanzania International Petroleum Reserves Limited (TIPER), Mhe. Ndejembi amesema kuna umuhimu wa kuweka mifumo imara ya usimamizi wa mafuta yanayoingia nchini.
Katika kikao hicho, Waziri Ndejembi ameielekeza PBPA kuweka mfumo madhubuti wa upangaji wa ratiba ya ushushaji wa mafuta (sequencing), ili kuhakikisha maghala yote yanayohusika na usambazaji yanapata mafuta kwa usawa na kwa wakati.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa mafuta katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuongeza ufanisi katika mnyororo wa usambazaji.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imekubaliana kuharakisha ushushaji wa meli za mafuta zinazoingia nchini, hususan zile za matumizi ya ndani, ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika na salama.
Mhe. Ndejembi amebainisha kuwa tayari Serikali imefanya mazungumzo na TIPER na kuelekeza kuwepo kwa utaratibu mzuri wa upangaji wa ushushaji wa mafuta, utakaozingatia usawa kwa wasambazaji wote.
Hata hivyo, amewataka wananchi kutokuwa na taharuki kuhusu upatikanaji wa mafuta, akisisitiza kuwa nchi ina akiba ya kutosha kukidhi mahitaji.
Kwa upande wake, EWURA imeelekezwa kuhakikisha kuwa mafuta yote yanayotoka kwenye maghala yanafika kwa walengwa na kutumika ipasavyo, huku vituo vya mafuta vikihimizwa kuuza bidhaa kulingana na mahitaji halisi ya soko.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER, Mohamed Mohamed na wataalam mbalimbali wa sekta ya mafuta.