The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

NDEJEMBI, UBALOZI WA SWEDEN NA...

NDEJEMBI, UBALOZI WA SWEDEN NA UJERUMANI WAJADILI FURSA ZA USHIRIKIANO SEKTA YA NISHATI.

Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi leo Mei 12, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Wawakilishi kutoka Ubalozi wa Sweden, Ujerumani na kampuni ya Siemens Energy kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya nishati nchini.

Mazungumzo hayo yalihusisha pia Taasisi ya kifedha ya KfW IPEX ya Ujerumani na EKN ya Sweden ambazo zimekuwa zikishiriki katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ya nishati.

Katika kikao hicho, ujumbe kutoka Siemens Energy uliwasilisha maeneo mbalimbali ambayo wameonesha nia ya kuwekeza ikiwemo uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia, ufadhili na usambazaji wa mitambo ya kuzalisha umeme ambapo ilieleza uzoefu na uwezo wa kampuni hiyo katika teknolojia za mitambo ya kuzalisha umeme.

Katika kikao hicho Waziri Deogratius Ndejembi alieleza kufurahishwa kwake na ujio wa ujumbe huo katika wakati ambao Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya nishati nchini.

Aidha, aliipongeza kampuni ya Siemens Energy kwa kupata kandarasi ya kusambaza mitambo ya kuzalisha umeme katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Mkuranga wenye uwezo wa kuzalisha megawati 177, akisema hatua hiyo inaonesha imani waliyonayo wawekezaji wa kimataifa kwa Tanzania.

Sambamba na hilo, Mhe. Deogratius Ndejembi alizihimiza kampuni hizo kuangalia fursa za kuwekeza katika vyanzo vingine vya uzalishaji umeme ikiwemo umeme wa jua, upepo na jotoardhi ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kufikia lengo la kuzalisha megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

Nao Wawakilishi wa mabalozi pamoja na kampuni hizo waliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuamini teknolojia ya Siemens Energy na ushirikiano wa kifedha kutoka katika nchi zao huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha upatikanaji wa mitambo na fedha za utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, Kamishna Msaidizi wa Umeme Mha. Styden Rwebangira, Kaimu Kamishna wa Petroli, Mha. Petro Marwa pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Nishati.