Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

Rais Dkt. Samia apokea taarifa...

Rais Dkt. Samia apokea taarifa ya utekelezaji wa REA III Mzunguko wa Pili nchi nzima

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika maeneo yote nchini.

Dkt. Samia amepokea taarifa hiyo wakati akizungumza na wananchi alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku tatu katika eneo la Shelui Mkoani Singida, Tarehe 17 Oktoba 2023.

Katika hotuba yake kwa wananchi alisema kuwa, asilimia 90 ya vijiji vyote nchini vimepata umeme na hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliyoelekeza kupeleka umeme katika vijiji vyote nchini kabla ya mwaka 2025.

Aidha alisema kuwa Serikali inafanya juhudi na mipango ya muda mfupi na mrefu kuimarisha umeme wa Gridi ya Taifa ili kuondokana na kero ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika.

“Tunaendelea kutekeleza ahadi zote zilizokuwa zinatolewa wakati tukiomba dhamana ya kuliongoza Taifa letu kupitia Chama cha Mapinduzi ili kuwahudumia watanzania na kuwaletea Maendeleo”, alisema Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kwa Serikali ilitoa shilingi Trilioni 1.57 ili kumaliza uunganishaji wa umeme katika Vijiji 4071 ambavyo vilikuwa havina Umeme kabla mwaka 2025.

Mradi huo ni wa kipekee sana kwa kuwa ulikutana na Uongozi wa Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na ulikuwa na Vijiji vingi kuliko awamu zote zilizotangulia.

“Mpaka sasa tumepeleka umeme katika vijijini vyote kwa asilimia 90, tunamuomba Mwezi Mungu Inshaallah, ifikapo mwezi Juni 2024, Mhe. Rais tutakuwa tumekukabidhi kazi uliotupatia ya kupeleka umeme kwenye vijiji vyote 4071 vilivyobakia nchi nzima”, alisisitiza Mhe. Kapinga.

Sambamba na hilo alisema Wizara pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini( REA) imetangaza vita kwa wakandari wote legelege na walioshindwa kutekeleza kazi kwa wakati kwa kuwanyima kazi.

Akizungumzia agizo lililotolewa Mhe. Rais, mwezi mmoja uliopita la kutokatika Umeme kwa kipindi cha Miezi 6, Mhe. Kapinga amesema kuwa, tayari wameimarisha mitambo ya Umeme iliyokuwa imepata hitilafu na kushindwa kuzalisha umeme ya Ubungo I na Tegeta ambayo mpaka sasa imeweza kuzalisha jumla ya Megawati 17.

Pia kuendelea na kazi ya kusimamia ukarabati wa mtambo wa Ubungo II wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 43 ili kuurejesha katika hali yake ya kawaida.

Vilevile kuwasha Mtambo wa kufua Umeme wa Rusumo wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 27.

Kuhusu Mradi wa Julius Nyerere, (JNHPP), Mhe. Kapinga amesema mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia 92.7 % ya utekelezaji wake na kazi inaendelea vizuri ili ifikapo Januari 2024 waanze majaribio ya kuzalisha umeme katika bwawa hilo.