SALOME AKUTANA NA WAWAKILISHI WA KAMATI TENDAJI KUTOKA TANZANIA NCHINI ETHIOPIA.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amekutana na kufanya kikao cha pembeni na wajumbe wa Kamati Tendaji (Steering Committee) ya Soko la Pamoja la Nishati Mashariki mwa Afrika (Eastern African Power Pool - EAPP), ya kutoka Tanzania waliopo nchini Ethiopia. Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kupokea ripoti na kupata uelewa wa kina wa masuala mbalimbali yaliyojadiliwa na kamati hiyo, ikiwa ni maandalizi muhimu kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa Ngazi ya Mawaziri.
Kamati hiyo tendaji imekuwa nchini Ethiopia tangu Julai 7, ambapo ilikuwa ikitekeleza kikao chake cha 37 cha maandalizi. Kikao hiki cha Naibu Waziri na kamati kimekuja wakati muafaka kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 8 na 9 Julai, ambapo maazimio na mikakati mbalimbali ya sekta ya nishati inatarajiwa kujadiliwa na kupitishwa.
Hatua hizi zote ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Mkutano wa 22 wa Baraza la Mawaziri la Soko la Pamoja la Nishati Mashariki mwa Afrika (Eastern African Power Pool - EAPP). Ushiriki wa Tanzania katika mikutano hii una umuhimu mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, biashara ya kuuziana umeme, kuunganisha gridi za Taifa na kuhakikisha usalama wa nishati kwa nchi wanachama wa ukanda huo.