Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​SEKONDARI YA MORINGE SOKOINE...

​SEKONDARI YA MORINGE SOKOINE YAPEWA ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Imeelezwa kuwa, familia nyingi nchini bado zinatumia kuni na mkaa kama vyanzo vikuu vya nishati safi ya kupikia, vyanzo ambavyo vina athari kubwa kwa afya, mazingira, na uchumi.

Kutokana na hilo, Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kama vile gesi, umeme na matumizi ya majiko banifu pamoja na kuhakikisha kuwa nishati hizo safi zinawafikia wananchi.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay wakati aliposhiriki mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Moringe Sokoine iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha akiwa ni mgeni rasmi.

Mlay amesema tafiti zinaonesha kuwa moshi wa kuni na mkaa unasababisha magonjwa ya mfumo wa hewa hasa kwa wanawake na watoto, pia ukataji miti kupita kiasi kwa ajili ya mkaa unachangia ukame na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Amesema matumizi ya kuni pia yana athari ikiwemo za kiuchumi na elimu kwani muda mwingi hutumika kutafuta nishati hiyo hivyo kupunguza muda wa kufanya shughuli za kiuchumi na kujisomea kwa wanafunzi.

"Ninawahimiza ninyi wahitimu kuwa mabalozi wa mabadiliko haya ya nishati safi ya kupikia, elimisheni familia zenu kuhusu faida za kupika kwa kutumia nishati safi, sambamba na hilo jifunzeni teknolojia mpya kama vile utengenezaji wa majiko banifu au miradi ya bayogesi kwa wafugaji na uzalishaji wa mkaa mbadala." Amesema Mlay

Kwa upande wao, Wanafunzi wa Moringe Sokoine, Wazazi na Wananchi wamemshukuru Mkurugenzi wa Nishati safi ya kupikia kwa kushiriki mahafali hiyo na kupata elimu ya Nishati safi ya Kupikia.#NishatiTupokazini.