Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​SERIKALI KUANZISHA OFISI MAAL...

​SERIKALI KUANZISHA OFISI MAALUM YA MRADI WA LNG. MAZUNGUMZO KUKAMILIKA DISEMBA - WAZIRI MAKAMBA.*

SERIKALI KUANZISHA OFISI MAALUM YA MRADI WA LNG. MAZUNGUMZO KUKAMILIKA DISEMBA - WAZIRI MAKAMBA.*

Waziri wa Nishati, January Makamba, ametembelea ofisi za Kampuni ya Shell, nchini Uholanzi, na kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa kampuni hiyo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na utekelezaji wa mradi wa LNG nchini. Katika mazungumzo hayo na Bwana Cederic Cremers, Makamu wa Rais anayeshughulikia miradi ya LNG na Bwana John Crocker, Makamu Rais wa Shell anayehusika na Mahusiano ya Serikali,

Waziri Makamba alielezea azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mazungumzo yanakamilika mwezi Disemba mwaka huu na hatua za utekelezaji zinaanza mara baada ya hapo.

Katika mikutano hiyo, Waziri Makamba pia alielezea mpango wa Serikali wa kuanzisha Ofisi Maalum ya Kusimamia Utekelezaji wa Mradi wa LNG (Tanzania LNG Office) mnamo mwezi Novemba mwaka huu kwa lengo la kuratibu, kuharakisha na kurahisisha hatua za utekelezaji wa mradi.

Mradi huo wa kuchakata na kusindika gesi asilia iliyogundulika katika bahari kuu Kusini mwa Tanzania, utaleta nchini uwekezaji wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 40, unatekelezwa na Makampuni ya Shell ya Uholanzi na Equinor ya Norway na washirika wao.

Waziri Makamba alieleza kwamba mradi huo una manufaa mengi kwa Tanzania na utafungua fursa nyingi kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini mwa Tanzania na kuiongezea mapato nchi na kuleta ajira na mapinduzi ya kiuchumi na kijamii nchini.

Kwa upande wa Kampuni ya Shell, Bw. Crocker, aliishukuru Serikali ya Awamu ya 6, inayoongwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa wawekezaji matumaini na kutoa kipaumbele katika mradi huo na kuwezesha kusainiwa kwa mkataba wa awali. Pia alieleza kuridhishwa kwao kwa hatua ya majadiliano iliyofikiwa katika maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo. Bw. Crocker alisisitiza nia yao na ya washirika wao ya kutekeleza mradi.