SERIKALI KUJENGA MTANDAO MKUBWA WA MABOMBA YA GESI-DKT.BITEKO
Asema lengo ni kurahisisha huduma kwa wananchi
Afanya mazungumzo na kampuni Rashal Energies inayojenga Bomba la Gesi
Kisemvule-Mbagala
Aikaribisha kampuni ya CNOOC kushiriki Duru a Tano Vitalu vya Mafuta
na Gesi Asilia
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Rashal
Energies, Farhiya Warsame ambayo inajenga Bomba la Gesi kutoka
Kisemvule hadi Mbagala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi ya
vituo vya Kujazia Gesi kwenye Magari (CNG) na kwenye viwanda.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam tarehe 06 Machi, 2025
kando ya Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAPCE’25) linalofanyika kwa Siku Tatu jijini Dar es
Salaam.
Dkt.Biteko amesema kuwa lengo la Serikali ni kuwa na mtandao mkubwa wa
mabomba ya gesi pamoja na vituo vya kujazia gesi kwenye magari ili
kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi.
Kutokana na hilo Dkt.Biteko ameeleza kuwa Serikali ipo tayari wakati
wowote kutoa ushirikiano kwa kampuni zinazotaka kuwekeza kwenye kutoa
huduma hiyo kwa wananchi.
Kwa upande wake, Bi.Farhiya Warsame amemshukuru Dkt.Biteko kwa
miongozo yake ambayo imepelekea kampuni hiyo kuanza kutekeleza mradi
huo.
Ameeleza kuwa wananchi wameonesha mwamko mkubwa kwenye kuendesha
vyombo vyao vya usafiri kwa kutumia gesi asilia badala ya mafuta
kutokana na gesi asilia kuwa na gharama nafuu kuliko mafuta.
Vilevile, Dkt. Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa
kampuni ya Rock Mountain ya nchini Canada, Bw. Nick Lenstra ambayo
imesaini Mkataba wa Ushirikiano na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) kwa ajili ya kuanza kazi za upembuzi yakinifu na
kuzungumza na wadau wa ndani ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA) ili kutumia gesi asilia kutengeneza nishati kwa njia ya
kimiminika ambayo inaweza kutumika kwenye ndege.
Hali kadhalika, Dkt.Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu
wa Rais wa kampuni ya CNOOC kwa upande wa Uganda, Wang Juteng ambapo
pamoja kuzungumzia Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini,
ameikaribisha kushiriki Duru ya Tano ya Kunadi Vitalu vya Mafuta na
Gesi Asilia nchini.