The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

SERIKALI YAONGEZA KASI YA MATU...

SERIKALI YAONGEZA KASI YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA NCHINI.

Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia Wizara ya Nishati, Ndg. Nolasco Mlay, amesema kuwa nishati safi ya kupikia ni suluhisho muhimu linalorahisisha maisha ya wananchi kutokana na usalama wake, gharama nafuu pamoja na manufaa yake kwa afya na mazingira.

Akizungumza katika kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, Mlay amesema nishati safi ya kupikia inahusisha teknolojia mbalimbali, ikiwemo gesi ya kupikia (LPG), umeme, biogesi, gesi asilia, majiko banifu na mkaa mbadala unaozalishwa kutokana na mabaki ya mazao ya kilimo na shughuli za viwandani.

Amefafanua kuwa gharama za matumizi ya nishati safi ya kupikia hutofautiana kulingana na teknolojia inayotumika na uwezo wa mtumiaji. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha wananchi wa makundi yote wanapata fursa ya kutumia nishati hizo kwa urahisi.

Mlay amebainisha kuwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Serikali imekuwa ikitoa majiko ya kupikia kwa bei ya ruzuku kwa lengo la kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususan katika maeneo ya vijijini.

Aidha, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Sambamba na hilo, Serikali inaendelea kusambaza huduma ya umeme hadi vitongojini na kuimarisha matumizi ya gesi asilia, hususan katika maeneo yenye miundombinu ya huduma hiyo.