The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

SERIKALI YATANGAZA FURSA ZA UW...

SERIKALI YATANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI NISHATI ZA DOLA BIL. 12.9

Serikali ya Tanzania imetangaza uwepo wa fursa kubwa za uwekezaji katika sekta ya nishati zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 12.9, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati nchini.

Akizungumza katika mjadala kuhusu ushirikiano wa Marekani na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa mkutano wa Powering Africa Summit Machi 20, 2026 jijini Washington DC, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema uwekezaji huo unahitajika katika maeneo mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme, usafirishaji, usambazaji pamoja na nishati safi ya kupikia.

Ameeleza kuwa katika sekta ya uzalishaji wa umeme, miradi 13 imepangwa kutekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo, ikihitaji uwekezaji wa dola bilioni 2.77, hatua itakayowezesha kuongeza megawati 1,421 za umeme nchini.

Kwa upande wa miundombinu ya usafirishaji wa umeme, amesema jumla ya miradi 23 yenye thamani ya dola bilioni 1.21 inapangwa kujengwa, ikiwemo kilomita 1,350 za njia za kusafirisha umeme pamoja na vituo vya kupozea umeme.

Aidha, Mhe. Salome amebainisha kuwa kuna fursa nyingi katika sekta ya gesi asilia, akieleza kuwa Tanzania ina zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 za gesi ambazo bado hazijatumika kikamilifu.

Amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika uchimbaji, usindikaji na matumizi ya gesi hiyo katika uzalishaji wa umeme na shughuli za viwandani.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikilenga kufikia asilimia 75 ya matumizi hayo ifikapo mwaka 2030. Mpango huo unahusisha usambazaji wa majiko bora, gesi pamoja na teknolojia nyingine rafiki kwa mazingira.

Mhe. Salome amewahimiza wawekezaji walioshiriki mkutano huo kutumia fursa zilizopo kuwekeza nchini, huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuweka sera rafiki kwa uwekezaji.

Katika Mkutano huo Naibu Waziri Salome ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Else Sia Kanza na wataalam kutoka Wizarani, TANESCO, REA pamoja na PURA.