The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

SERIKALI YAWAPONGEZA WADAU WA...

SERIKALI YAWAPONGEZA WADAU WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Serikali kupitia Wizara ya Nishati imewapongeza wadau wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali zinazolenga kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, tarehe 04 Februari, 2026, wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia katika Shule ya Sekondari ya Bunge, jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mataragio alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wadau mbalimbali wanaoshirikiana katika kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia, ikiwemo kampuni za ORYX na ENVOTEC, ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya mifumo ya kupikia katika shule hiyo.

“Ninawapongeza wadau wote wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia. Ushirikiano huu ni muhimu katika kufanikisha ajenda ya kitaifa ya kulinda afya za wananchi na mazingira,” alisema Dkt. Mataragio.

Amefafanua kuwa ni agizo la Serikali kuhakikisha taasisi zote zinazohudumia au kutumia watu zaidi ya 100 zinatumia nishati safi ya kupikia, hatua itakayosaidia kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Aidha, Dkt. Mataragio alieleza kuwa inakadiriwa takribani watu milioni 2.3 hufariki dunia kila mwaka kutokana na athari za hewa chafu inayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.

Changamoto hiyo inaathiri zaidi wanawake na watoto wa kike katika maeneo mbalimbali duniani.

Aliongeza kuwa matumizi ya nishati isiyo salama husababisha pia wananchi kutumia muda mwingi kuandaa chakula pamoja na muda mrefu kutafuta kuni na mkaa, hali inayochangia kupungua kwa tija ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua kubwa za kisera na kifedha ili kubadilisha mtazamo wa wananchi na kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Juhudi zinazoendelea ni pamoja na kuongeza uzalishaji na usambaji wa umeme, usambaza miundombinu ya gesi asilia pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala za nishati safi.