SHULE YA SEKONDARI NJOMBE YAOKOA MIL.9/- KWA KUACHANA NA KUNI.
Shule ya sekondari njombe imeokoa zaidi ya sh. Milioni tisa kwa muhula baada ya kuachana na matumizi ya kuni na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.
Mkuu wa shule hiyo, benard william, amesema hatua hiyo imetokana na utekelezaji wa maelekezo ya serikali yanayohamasisha matumizi ya nishati safi na salama katika taasisi mbalimbali, ikiwemo shule.
Akizungumza wakati wa ziara ya wataalamu kutoka wizara ya nishati shuleni hapo, william ameeleza kuwa hapo awali shule ilikuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kununua kuni, hali iliyokuwa ikiathiri bajeti ya uendeshaji wa shule.
Amesema matumizi ya nishati safi yamepunguza gharama kwa kiwango kikubwa, sambamba na kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa jikoni.
“mbali na kupunguza gharama, nishati safi imeongeza ufanisi katika upishi kwani inapika kwa haraka zaidi na kwa usalama ukilinganisha na matumizi ya kuni,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa hatua hiyo imeondoa changamoto ya moshi uliokuwa ukiathiri afya za wapishi, hivyo kuboresha ustawi wao kazini.
Kwa upande wake, mjiolojia wizara ya nishati, kitengo cha nishati safi ya kupikia, nsajigwa maclena, amesema wizara inaendelea kuhamasisha taasisi mbalimbali kuachana na matumizi ya nishati zisizo salama kama kuni na mkaa.
Ameeleza kuwa lengo la serikali ni kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti na kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanaongezeka nchini.
Nsajigwa ameipongeza shule hiyo kwa kuchukua hatua hiyo, akisema ni mfano mzuri kwa taasisi nyingine kuiga katika utekelezaji wa sera ya serikali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.