Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

TANZANIA NA UGANDA ZATIA SAINI...

TANZANIA NA UGANDA ZATIA SAINI MKATABA MAHSUSI KWA AJILI YA UPEMBUZI YAKINIFU UJENZI WA BOMBA LA GESI

DKT BITEKO ASEMA NI KIELELEZO CHA USHIRIKIANO WA NCHI HIZO MBILI


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya
Uganda zimetia saini mkataba mahsusi utakaowezesha kuanza kwa kazi ya
upembuzi yakinifu wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi
kutoka Tanzania kwenda Uganda.

Mkataba huo umesainiwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Dkt. Doto Biteko pamoja na Mhe.
Ruth Nankabirwa, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Jamhuri
ya Uganda.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko amesema kuwa,
kusainiwa kwa Mkataba huo kumetokana na Makubaliano ya Awali
(Memorandum of Understanding - MoU) kati ya nchi hizi mbili
yaliyosainiwa mwezi Agosti, mwaka 2018 kwa ajili ya ujenzi wa Bomba
la kusafirisha Gesi Asilia kutoka Tanzania kwenda Uganda kutokana na
Tanzania kugundua kiasi kikubwa cha gesi katika kina kirefu cha bahari
na nchi kavu.

“ Nchi hizi mbili zimekubaliana kufanya kazi ya upembuzi yakinifu kwa
pamoja kuwezesha tathmini ya mradi na kutoa muongozo wa uwezekano wa
mradi ikiwemo muundo wa mradi, mahitaji ya gesi, ukubwa wa bomba na
taarifa nyingine muhimu zinazohusu mradi huo kwa ajili ya kufanya
maamuzi.” Amesema Dkt. Doto Biteko

Dkt. Biteko amesema kuwa, Nishati ni ufunguo wa maendeleo kwa nchi
yoyote ile duniani na umoja ni nguvu hivyo ametoa wito kwa nchi hizi
mbili kutumia fursa ya kutekeleza mradi huu ambao utaunganisha nchi
hizi mbili katika nyanja ya kiuchumi na kijamii.

Amesema kuwa, licha ya Tanzania kugundua kiasi kikubwa cha gesi asilia
takiriban futi za ujazo trilioni 57.54, mahitaji ya rasilimali hii
yanakua kwa kasi ndani na nje ya nchi na hii inapelekea Serikali
kuweka nguvu zaidi katika utafutaji kwa lengo la kuongeza upatikanaji
wa nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Eyasi Wembere, Mnazi
Bay Kaskazini, Songosongo Magharibi, Ziwa Tanganyika na katika kina
kirefu cha maji baharini.

Ameongeza kuwa, Tanzania inaendelea kutafuta wabia wa kimkakati
watakaoweza kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) ili kutafiti na kuendeleza vyanzo vya upatikanaji wa mafuta na
gesi.

Pamoja na kupongeza timu zilizofanya kazi hadi kupelekea kusainiwa kwa
mkataba huo, ameagiza kuwa kazi zilizopangwa kufanyika baada ya
kusainiwa kwa mkataba huo zifanyike kwa wakati ikiwemo upatikanaji wa
Mshauri Mwelekezi wa kufanya kazi hii na kila upande unapaswa kuona
kuwa mradi huo ni wa kipaumbele.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini kutoka
nchini Uganda Mhe. Ruth Nankabirwa amesema kuwa, Uganda inatambua
umuhimu wa mradi huu na kuongeza kuwa kumekuwepo na mahitaji makubwa
ya matumizi ya gesi hivyo wana kila sababu ya kuhakikisha kunakuwepo
na uharakishwaji wa mradi huo.

Ameitaka Kamati ya pamoja ya utekelezaji wa Mradi huo kuhakikisha
wanaharakisha mchakato wa manunuzi ya Mshauri Mwelekezi wa mradi ili
kuharakisha upembuzi yakinifu tayari kwa utekelezaji.

Aidha, amesema Tanzania na Uganda zimekuwa zikishirikiana katika
miradi mbalimbali kwenye sekta ya Nishati ikiwemo Mradi wa uzalishaji
wa umeme wa maji Megawati 14 wa Kikagati, mradi wa kusafirisha umeme
kutoka Masaka Mutukula hadi Mwanza na mradi wa Bomba la Mafuta ambalo
waliona lipite Tanzania.

Hafla hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makatibu
Wakuu wa Wizara za Nishati kutoka nchi zote mbili, makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Balozi wa Uganda
nchini Tanzania, Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara hizo ikiwemo
TPDC, EWURA, PURA na UNOC na wawakilishi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.