TANZANIA NI NJIA YA USAFIRISHAJI MAFUTA YA UGANDA KUPITIA MRADI WA EACOP.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema ushiriki wa Tanzania kwenye Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) upo kwenye biashara ya kusafirisha mafuta ghafi tu (transit nation) kutoka Kabaale Hoima hadi Chongoleani, Tanga na baadaye kupelekwa kwenye masoko ya kimataifa.
Mhe. Salome ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma Aprili 14, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Mhe Kenneth Nollo aliyehoji Serikali ina mpango gani wa kuanza kusafirisha mafuta ghafi yanayotoka Uganda kupitia Bomba la Mafuta EACOP.
Mhe. Salome amesema mikataba ya mauzo hayo imeingiwa kati ya wabia wa mkondo wa juu nchini Uganda ambao ni Serikali ya Uganda na Makampuni ya Kimataifa (Totalenergies) kutoka Ufaransa na CNOOC kutoka China kwa kuzingatia vigezo vya usanifu wa kitaalam na uwezo wa uzalishaji wa visima.
“Mhe. Spika naomba ifahamike pia, kwenye hii biashara tayari mikataba ya mauzo ya mafuta hayo imeshaingiwa kati ya wabia wa mkondo wa juu (upstreamers) na wanunuzi (masoko ya kimataifa),” Amesema Mhe. Salome.