TANZANIA YAJIPANGA KUNUFAIKA NA GESI TRILIONI 57.54, WAWEKEZAJI WAALIKWA.
Tanzania imeingia katika hatua mpya ya maendeleo ya sekta ya gesi asilia kufuatia kuthibitishwa kwa uwepo wa akiba kubwa inayokadiriwa kufikia futi trilioni 57.54, hatua inayotarajiwa kubadilisha mwelekeo wa uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika mkutano wa Powering African Summit jijini Washington Dc Machi 21,2026, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema rasilimali hiyo kubwa inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye fursa kubwa zaidi za uwekezaji katika nishati barani Afrika.
Amesema pamoja na mafanikio hayo, takribani asilimia 70 ya maeneo yenye uwezekano wa kuwa na mafuta na gesi bado hayajachunguzwa, jambo linalotoa nafasi kubwa kwa wawekezaji kushiriki katika shughuli za utafutaji na uchimbaji.
Mhe Salome alifafanua kuwa Serikali ipo katika hatua za maandalizi ya kuanzisha msimu mpya ya utoaji wa vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi ikiwa ni mkakati wa kuvutia wawekezaji wapya na kuongeza uzalishaji wa rasilimali hizo.
Aidha aliongeza kuwa Tanzania sasa inaelekea kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya gesi ikiwemo mradi wa kuchakata Gesi kuwa kimiminika (LNG), unaotarajiwa kufungua masoko ya kimataifa na kuongeza pato la taifa.
Serikali inalenga kuhakikisha gesi asilia inatumika zaidi ndani ya nchi kwa ajili ya kuzalisha umeme, kuendesha viwanda, matumizi ya majumbani pamoja na matumizi ya usafiri ili kuongeza thamani ya rasilimali hiyo’ amesema.
Aidha, aliongeza kuwa uwekezaji unahitajika katika miundombinu muhimu ikiwemo mabomba ya kusafirisha gesi, vituo vya kujaza gesi na mifumo ya usambazaji ili kufanikisha matumizi mapana ya nishati hiyo safi hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuja Tanzania na kuwekeza miradi hii ambayo si tu kwamba itanufaisha Taifa letu bali hata wawekezaji pia watanuika kuwa kama nchi tumeweka mazingira bora ya uwekezaji yenye uwazi na uhakika.
Aliongeza kuwa matumizi ya gesi asilia yatapunguza gharama za uzalishaji viwandani na kusaidia kulinda mazingira kwa kupunguza utegemezi wa nishati isiyo safi kama kuni na mkaa.
Hatua hizi zinatarajiwa kuiwezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na utajiri wa gesi asilia, kuongeza ajira, na kuimarisha uchumi wa taifa katika kipindi kijacho.