The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

TANZANIA YAPIGA HATUA MAANDALI...

TANZANIA YAPIGA HATUA MAANDALIZI YA UWEKEZAJI WA NISHATI YA NYUKLIA

Tanzania imeendelea kupiga hatua katika maandalizi ya uwekezaji na uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia, baada ya Serikali kukamilisha hatua kadhaa za awali ikiwemo mpango mkakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Hatua hiyo imeelezwa leo Februari 2, 2026 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi

Mramba, wakati wa kikao kati ya Wizara hiyo na ujumbe kutoka Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Nishati ya Nyuklia (IAEA), kilichofanyika Wizara ya Nishati, Mtumba.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Mramba amesema Tanzania imefanikiwa kukamilisha mahitaji muhimu yanayohitajika kuelekea uwekezaji huo, ikiwemo kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji (Road Map) wa miaka sita na nusu.

Ameeleza kuwa mpango huo pia unahusisha kutoa elimu na mafunzo kwa wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambayo tayari imeunda kitengo maalumu cha kusimamia uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia na kupendekeza mafunzo hayo yafanyike Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mhandisi Mramba ameishukuru IAEA kwa kuendelea kutoa ushauri na muongozo wa kitaalamu tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliporidhia mpango wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia nchini.

Kwa upande wake, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, amesema Tanzania imepiga hatua katika maeneo mbalimbali ikiwemo kukamilisha mapitio ya Road Map, kufanya vikao vya NEPIO vilivyopelekea kuundwa kwa Kamati maalumu, pamoja na kuwasilisha nyaraka za utekelezaji katika Sekretarieti ili kupata idhini ya Serikali.

Naye, Mkurugenzi wa IAEA, Cashaw C Wolde, amesema kuna umuhimu wa kuwakutanisha wataalamu wabobevu wa nyuklia ili kuimarisha zaidi mchakato huo, akibainisha kuwa endapo uwekezaji huo utakamilika, Tanzania itanufaika kwa kupata umeme wa uhakika na wa kutosha.

Amesema nishati ya nyuklia ni chanzo cha umeme chenye nguvu

kitakachosaidia upatikanaji wa nishati ya uhakika.