Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Tathmini ya upelekaji umeme m...

​Tathmini ya upelekaji umeme mijini kwa sh.27,000 kufanyika ndani ya miezi mitatu

Tathmini ya upelekaji umeme mijini kwa sh.27,000 kufanyika ndani ya miezi mitatu

Na Teresia Mhagama, Songwe

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amesema kuwa tathmini ya agizo la Serikali la kupeleka umeme mijini na vijijini kwa shilingi 27,000 itafanyika ndani ya miezi mitatu ili kuona kama agizo hilo linatekelezwa ipasavyo.

Waziri wa Nishati alisema hayo tarehe 27 Agosti, 2021 wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe wakati akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Cosmas Ishenye, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidarya na Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole kabla ya kuzindua kimkoa mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili.

“ Suala la kupelekewa umeme kwa zaidi ya shilingi 27,000 halipo, pia suala la mwananchi kuuziwa nguzo halipo, mtu awe tajiri au maskini bei ni moja tu ambayo ni shilingi 27,000 tu hivyo tutafuatilia kuona kama agizo hili linafanyiwa kazi na watendaji wetu.” Alisema Dkt. Kalemani

Alisema Serikali inataka wananchi wengi waunganishiwe umeme ili wautumie kwa shughuli mbalimbali hivyo aliwaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuongeza kasi ya kusambaza umeme na kuacha kuweka vikwazo vya kumpelekea mwananchi umeme kama vile malipo ya nguzo.

Akizungumzia hali ya upatikanaji umeme kwa Mkoa wa Songwe alisema kuwa, kwa sasa Mkoa huo umejengewa kituo kidogo cha kupoza umeme wakati Serikali ikifanya jitihada nyingine za kupeleka umeme wa uhakika mkoani humo.

Aliongeza kuwa, kuna mradi mkubwa wa kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Iringa, kupitia Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga ambao utaimarisha zaidi hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa hiyo pamoja na Songwe ambapo mkandarasi anatarajiwa kuanza kazi mwezi Februari mwakani.

Akiwa wilayani Mbozi, Waziri wa Nishati alikagua kituo kidogo cha kupoza umeme wilayani humo na kuiagiza TANESCO kuanza kupeleka umeme kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo ndani ya siku Kumi baada ya wananchi hao kulalamika kuwa hawana umeme.

Awali, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Songwe, Grace Mtungi alisema kuwa mahitaji ya juu ya umeme mkoani humo ni megawati 13.5 huku uwezo wa mitambo ya umeme ukiwa ni megawati 15 hivyo Mkoa huo unapata umeme wa kutosha mahitaji kwa sasa.

Aliongeza kuwa, idadi wa wateja waliounganishwa na umeme inaendelea kuongezeka kwani katika mwaka 2019/2020 wateja waliounganishwa umeme walikuwa ni 51,176 na kwa sasa kuna wateja 58,587.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati alizindua Mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Songwe ambao unatarajiwa kusambaza umeme katika Vijiji 127 kwa gharama ya shilingi bilioni 42.3.

Katika uzinduzi huo, Waziri wa Nishati aliitaka kampuni ya Derm Electrics kufanya kazi ya usambazaji umeme mkoani humo kwa muda wa miezi 18 kwa kutumia vifaa vinavyopatikana nchini.

Kuhusu hali ya usambazaji umeme vijijini nchini, alisema kuwa, mpaka sasa takriban vijiji 10,312 vimeshasambaziwa umeme na vimebaki vijiji 1956 huku lengo likiwa ni Vijiji vyote kuwa na umeme ifikapo Disemba mwakani.