Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​TPDC, Baker Botts waingia mka...

​TPDC, Baker Botts waingia mkataba majadiliano LNG

Na Janeth Mesomapya

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Baker Botts (UK) LLP wamesaini Mkataba wa Huduma ya Ushauri wa Kitaalam na Kampuni ya Baker Botts (UK) LLP ya Uingereza ili kushirikiana na Serikali katika majadiliano ya kutekeleza Mradi wa kubadili Gesi asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG).

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo ilifanyika Januari 25, 2022 jijini Arusha huku ikishuhudiwa na Waziri wa Nishati January Makamba, Mwenyekiti wa Majadiliano kwa upande wa Serikali ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi Charles Sangweni, viongozi wa Serikali, na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati nchini.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo, Waziri Makamba alisema kuwa kampuni hiyo ya Baker Botts ni kampuni kubwa ya kisheria na kitaalamu ambayo imebobea katika kutoa ushauri wa masuala ya mafuta na gesi kwenye nchi mabalimbali duniani.

“Baada ya kusaini mkataba huu, imani yetu ni kwamba mazungumzo haya yataenda haraka na kwa ufanisi zaidi na Serikali itapata mkataba ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu,” alieleza Waziri Makamba

Aidha, alieleza kuwa majadiliano kuhusu uwekezaji wa LNG baina ya Serikali na washirika wa mradi huo yanaendelea vizuri na kwamba kuna matumaini makubwa kuwa mradi huo utafanikiwa huku pande zote mbili zikikubaliana kuhusu haja ya kuharakisha mazungumzo hayo huku wakizingatia ufanisi, weledi na uangalifu mkubwa.

Waziri Makamba aliongeza kuwa majadiliano hayo yanahusu manufaa yatakayotokana na mradi huo wa LNG ikiwa ni pamoja na kipato kwa serikali, uwezo wa Watanzania kuijua sekta pamoja na ushirikishwaji wa wazawa katika kutoa huduma na bidhaa katika kipindi kizima cha utekelezwaji wa mradi.

“Mradi huu pia utasaidia kuiingiza Tanzania katika ramani ya dunia ya nchi zenye nguvu ya ushawishi kutokana na kuwa na nishati ambayo inatumika na inahitajika duniani,” aliongeza.

Alibainisha pia kuwa manufaa mengine ni pamoja na gesi itakayozalishwa kutumika katika kumaliza changamoto ya uzalishaji wa umeme nchini kutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha gesi asilia.

Kwa upande wake Mha. Sangweni alieleza kuwa majadiliano hayo yamejikita katika maeneo makuu manne ambayo ni ya kisheria, kiufundi, kiuchumi pamoja na eneo la masoko.

“Serikali imedhamiria kutekeleza mradi huu na tumepewa muda wa mwaka mmoja kuhakikisha tumefikia muafaka wa majadiliano haya baina ya serikali na wawekezaji wa mradi huu,” aliongeza.

Mradi wa LNG unakadiriwa kuwa wa thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 30 huku wabia wake wakuu wakiwa ni kampuni za Equinor, Shell na TPDC kwa niaba ya serikali ambao ni waendeshaji wa vitalu namba 1, 2 na 4.