The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

TUMEONDOA VAT KATIKA UAGIZAJI...

TUMEONDOA VAT KATIKA UAGIZAJI WA MITUNGI YA GESI ILI KURAHISISHA UPATIKANAJI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA WANANCHI- MHE. NDEJEMBI

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kuwa Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye uagizaji wa mitungi ya gesi (LPG), mitungi mikubwa ya gesi (LPG bulk facility) pamoja na carbonizers za kutengeneza mkaa mbadala ikiwa ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Serikalikupunguza bei na kurahisisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo Machi 17, 2026 Wilayani Morogoro, Mkoa wa Morogoro wakati akifungua Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililoandaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi likihusisha Wizara na Taasisi mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Taasisi za kifedha, Asasi za kiraia pamoja na wazalishaji, wasambazaji na watumiaji wa nishati safi ya kupikia.

“Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka kipaumbele katika kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa wananchi kupitia upatikanaji wa mitungi ya gesi, majiko banifu, gesi vunde na kupitia usambazaji wa umeme hadi ngazi ya vitongoji ambao unawezesha matumizi ya nishati ya umeme katika kupikia. Mpaka sasa TANESCO kupitia kampuni ya MECS imewezesha wateja 480 kupata majiko ya kupikia kwa umeme kwa kulipia kidogokidogo kupitia bili za umeme.” Amesema Mhe.Ndejembi

Ameeleza kuwa, mikakati ya Serikali ya kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034 na asilimia 75 ifikapo 2030 itawezekana endapo wadau wote watashirikiana, akisema kuwa tayari mwanga wa kufikia malengo hayo umeanza kuonekana kwani wakati Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unazinduliwa mwaka 2024, ni asilimia 6 tu ya Watanzania walikuwa wakitumia nishati safi ya kupikia na sasa hatua imepigwa hadikufikia asilimia 23.2.

Katika kongamano hilo, Waziri Ndejembi amewasisitiza wadau wote kuweka nguvu katika kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu nishati safi ya kupikia na hivyo kuleta mabadiliko ya tabia na mitazamo hasi juu ya nishati hiyo.

Pia amewataka kuongeza ubunifu na upanuzi wa miundombinu ya usambazaji wa nishati safi ya kupikia akieleza kuwa matumizi ya kuni na mkaa bado yanachangia zaidi ya asilimia 50 ya nishati ya kupikia kwenye kaya nyingi nchini.

Vilevile, ametaka Kongamano hilo la nishati safi ya kupikia litumike kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali, Sekta binafsi na asasi za kiraia ili kutanua wigo wa upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia kwa kuwa nishati hiyo ni muhimu kiafya, kimazingira, kiuchumi na katika usawa wa kijinsia.

kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema ajenda ya nishati safi ya kupikia ni kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wananchi hivyo amemshukuru Rais, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuifanya ajenda hiyo kuwa ni ya kitaifa huku akiwaasa wananchi wote kuiunga mkono.

Aidha, ameishauri Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo taasisi za fedhakuwawezesha wajasiriamali mkoani Morogoro kutumia fursa ya upatikanaji wa pumba zinazotokana na mpunga mkoani humo kutengenezea mkaa mbadala kutokana na wingi wa upatikanaji wake.

Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Bw. Nolasco Mlay amesema kongamano hilo linatoa fursa ya kipekee kwa wadau kutoka sekta za umma, binafsi, asasi za kiraia, pamoja na washirika wa maendeleo wa kimataifa kushirikiana, kubadilishana uzoefu, na kujadili mikakati ya kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadari Singo alisema dhumuni la kufanyika kwa kongamano la nishati safi ya kupikia mkoani Morogoro ni pamoja na kukuza uelewa wa manufaa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kiafya, kimazingira na kiuchumi pamoja na kuhamasisha mashirikiano baina ya Serikali, Sekta binafsi na asasi za kiraia.

Aliongeza kuwa, kongamano hilo pia limelenga kuainisha changamoto, utatuzi pamoja na fursa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.