The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

TUNAIMARISHA UZALISHAJI NA USA...

TUNAIMARISHA UZALISHAJI NA USAMBAZAJI UMEME KUKIDHI MAHITAJI YA UCHUMI UNAOKUA - MHANDISI MRAMBA.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, ameieleza Jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kimkakati kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usimamizi wa umeme ili kukidhi mahitaji ya uchumi unaokua kwa kasi.

Amesema hayo katika mkutano wa Bharat Electricity Summit 2026 unaofanyika nchini India.

“Tanzania inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuzalisha, usafirishaji na usambazaji umeme, lengo letu ni kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa kutosha kwa ajili ya matumizi ya kijamii na kukidhi mahitaji ya kiuchumi ambayo yanazidi kukua kwa kasi, kielelezo cha hatua tunazochukua ni pamoja na utekelezaji wa mradi wa umeme jua wa Kishapu wenye uwezo wa megawati 150, ambao awamu yake ya kwanza imekamilika na kuzalisha megawati 50.” Amesema Mhandisi Mramba

Aidha, ametaja mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa megawati 2,115 kuwa ni nguzo muhimu katika kuongeza uzalishaji wa umeme wa uhakika nchini.

Katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya nishati, Mhandisi Mramba amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kama sehemu ya mkakati wa kuharakisha maendeleo ya sekta hiyo.

Vilevile amesema kuwa, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya njia za kusafirisha umeme pamoja na kuunganisha gridi ya taifa na nchi jirani, hatua inayotarajiwa kuongeza usalama wa nishati kupitia biashara ya umeme ya kikanda.

Katika mkutano huo Mhandisi Mramba amesisitiza umuhimu wa maboresho ya gridi (grid modernisation) pamoja na matumizi ya teknolojia za smart grid, akieleza kuwa Tanzania tayari imeanza safari ya kuelekea katika mifumo hiyo ili kuongeza ufanisi, uthabiti na usalama wa huduma ya umeme.

Vilevile amegusia suala la nishati jadidifu linavyozidi kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa umeme akitanabaisha kuwa kuna haja kwa taasisi za mipango na mashirika ya umeme kuimarisha uwezo wa kiufundi na kiutendaji ili kuendana na mabadiliko ya mfumo huo wa kisasa.

Mkutano huo umewakutanisha viongozi na wataalam wa sekta ya nishati kutoka mataifa mbalimbali duniani kujadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya umeme, kukuza ushirikiano wa kikanda na kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta hiyo.