The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

UCHORONGAJI VISIMA VYA GESI AS...

UCHORONGAJI VISIMA VYA GESI ASILIA MTWARA WALETA NEEMA

Mradi wa uchorongaji wa visima vitatu vya gesi asilia unaotekelezwa katika Kitalu cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara, umeelezwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kupitia ongezeko la uzalishaji wa gesi, ajira na fursa za biashara.

Mhandisi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Fabian Mwose, ameyasema hayo wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa maendeleo ya mradi huo unaohusisha uchorongaji wa visima viwili vya uzalishaji na kimoja cha utafutaji.

Amesema mradi huo ulianza Februari 6, 2026 na hadi Juni 5 mwaka huu, visima viwili vya uzalishaji vilivyopewa majina ya MB5 na MS2 vilikuwa vimekamilika, huku uchorongaji wa kisima cha tatu cha utafutaji, KASA-1X, ukiendelea.

Kwa mujibu wa Mwose, moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia kutoka Kitalu cha Mnazi Bay.

Amesema kisima cha MB5 tayari kimeongeza uzalishaji kwa wastani wa futi za ujazo milioni 40 za gesi kwa siku, huku kisima cha MS2 ambacho bado kinafanyiwa majaribio kikitarajiwa kuongeza kiwango kingine kikubwa cha uzalishaji.

“Ongezeko hili limewezesha upatikanaji wa gesi zaidi kwa matumizi ya kuzalisha umeme, viwandani, kwenye vyombo vya usafiri kama magari na bajaji, pamoja na matumizi ya majumbani,” amesema.

Mbali na kuongeza uzalishaji wa nishati, Mwose amesema mradi huo umefungua fursa za ajira kwa Watanzania na kuongeza ushiriki wa wazawa katika sekta ya mafuta na gesi.

Amebainisha kuwa zaidi ya Watanzania 320 wameajiriwa katika nafasi mbalimbali za mradi huo, huku kandarasi za utoaji huduma na bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 20 zikielekezwa kwa kampuni na watoa huduma wa ndani.

Kwa upande wa uwekezaji, amesema utekelezaji wa mradi huo pamoja na miradi mingine ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia unaendelea kuongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuhusu fursa zilizopo katika sekta hiyo nchini.

Mwose amesema kukamilika kwa visima hivyo vitatu kutafanya idadi ya visima vilivyochorongwa nchini tangu kuanza kwa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia kufikia 99, kutoka visima 96 vilivyokuwepo awali.