UKIKAMATWA UMEFICHA MAFUTA: NI KESI YA UHUJUMU UCHUMI.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Huduma za Maji (EWURA) kuendesha operesheni ya kuwabaini watu wanaojihusisha na vitendo vya kuficha mafuta kwa makusudi ili kusababisha uhaba katika maeneo mbalimbali.
Ameeleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanatumia mwanya wa hali iliyopo kwa kuchukua mafuta kutoka kwenye maghala (depots) kwa kiwango kikubwa kuliko mahitaji yao, kisha kuyahifadhi wakisubiri bei mpya zitangazwe ndipo wayauze kwa bei ya juu.
Amesisitiza kuwa vitendo hivyo ni kosa la uhujumu uchumi, na yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria. Hivyo, amewaonya wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja kwa kuwa vinachangia kuleta uhaba wa mafuta.
“Nimewaelekeza Ewura kuanzia leo, usimwonee mtu yoyote aibu kama mtu akikamatwa ameficha mafuta, kwakweli sisi hatutamvumilia na Kamshna msimamie hilo mafuta yanayopakiwa hapa Dar es salaam muhakikishe yanafika kwenye vituo kama inavyokuwa imepangwa” amesisitiza Matarajio.
Dkt. Mataragio amefafanua kuwa tayari wameanza kupokea taarifa za baadhi ya vituo kukosa mafuta, hali inayochangiwa na vitendo vya aina hiyo ambapo mafuta yanapochukuliwa Dar es Salaam hayafiki katika vituo kama inavyotakiwa.
Kwa upande wake, Kamishna wa Mafuta na Gesi kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Goodluck Shirima, amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa usafirishaji na uuzaji wa mafuta nchini, ili kuhakikisha mafuta yote yanayopakiwa kutoka kwenye matenki yanafika katika vituo husika na wananchi wanaendelea kupata huduma bila usumbufu wowote.