The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

UTEKELEZAJI MKAKATI MATUMIZI B...

UTEKELEZAJI MKAKATI MATUMIZI BORA YA NISHATI YA UMEME KUANZA JULAI MOSI.

Serikali itaanza utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Ufanisi wa Nishati, Julai Mosi mwaka huu ili kuimarisha matumizi bora ya umeme na kupunguza gharama kwa watumiaji.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mdahalo wa ngazi ya juu kuhusu viwango vya chini vya ufanisi wa nishati (MEPS) na uwekaji wa lebo za nishati, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kufanikisha matumizi sahihi ya nishati.

Amesema Serikali inatambua ufanisi wa nishati kama nguzo muhimu ya maendeleo, ikichangia kupunguza gharama za umeme kwa wananchi, kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku ikiwezesha ukuaji wa uchumi endelevu.

Kwa mujibu wa Luoga, chini ya Mkakati wa Taifa wa Ufanisi wa Nishati (NEES 2024–2034), Serikali imeweka kipaumbele katika utekelezaji wa viwango vya MEPS na uwekaji wa lebo za nishati kwa vifaa vinavyotumika kwa wingi majumbani na viwandani, ikiwemo viyoyozi, majokofu, televisheni na mota za umeme.

Amebainisha kuwa utekelezaji huo unahusisha taasisi mbalimbali za udhibiti, zikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambazo zitakuwa na jukumu la kusimamia ubora wa bidhaa, kufanya upimaji wa viwango na kuhakikisha vifaa vinavyouzwa vinakidhi matakwa ya ufanisi wa nishati.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuondoa sokoni vifaa visivyo na ufanisi, huku ikiwarahisishia watumiaji kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa.

Aidha,ameeleza kuwa itapunguza ongezeko la mahitaji ya umeme na hivyo kupunguza gharama za uwekezaji katika uzalishaji wa nishati.

Hata hivyo, ametaja changamoto zinazoweza kujitokeza kuwa ni pamoja na uelewa mdogo kwa wadau, uhaba wa miundombinu ya upimaji na gharama za awali kwa wazalishaji.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali imepanga kuimarisha mifumo ya udhibiti, kuongeza uwezo wa taasisi husika ikiwemo TBS, pamoja na kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa wa matumizi bora ya nishati.

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha utekelezaji wenye mafanikio.

Kamishna Luoga amewashukuru washirika wa maendeleo kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya nishati nchini.