Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME WA...

UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE (JNHPP) WAFIKIA ASILIMIA 94.78

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2,115 kwa sasa umefikia asilimia 94.78 huku mashine mbili za kuzalisha umeme zikiwa tayari zimeshafungwa kwa ajili ya kuanza kuzalisha umeme.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 28 Desemba 2023 wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi huo wilayani Rufiji akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mwenyekiti wa Kamati aliyoteua Rais ya ufuatiliaji mradi wa JNHPP, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.

" Hatua iliyopigwa ya utekelezaji wa mradi huu kila mtu ameona kuwa ni kubwa kwenye hatua zote, mfano kwenye ujazaji maji wa bwawa la kuzalisha umeme, maji yamejaa kwa kiwango ambacho yanaruhusu kuzalisha umeme, pia ufungaji wa mashine ambazo zitatumika kuzalisha umeme, nafurahi kusema kuwa mashine mbili zimeshafungwa ambazo ni mashine namba Tisa na namba Nane na tunaamini kwamba mashine nyingine zitaendelea kufungwa kadri muda unavyoenda ili kupata megawati zote 2,115." Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amesema kuwa, kufungwa kwa mashine hizo mbili kunatoa matumaini ya kutekeleza agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kupunguza changamoto za umeme nchini ndani ya miezi Sita ambapo sasa imebaki miezi mitatu ya utekelezaji wa agizo hilo kwani mashine hizo zitazalisha megawati 470 na kuingizwa katika gridi ya Taifa ili kuongeza kiwango cha umeme.

Ameeleza kuwa, mashine namba Tisa itakapofika tarehe 2 Januari majaribio ya kwanza yajulikanayo kama dry testing yatakuwa yamekamilika na ifikapo mwezi Februari tarehe 19 majaribo ya pili yajulikanayo kama wet testing yatakuwa yamekamilika tayari kwa kuanza kuzalisha umeme na kwa mashine namba Nane matarajio ni kuwa, na yenyewe majaribio yakamilike mwezi Februari 2024.

Kuhusu ujazaji maji amesema kuwa, ujazo wa maji katika Bwawa la kuzalisha umeme ni mita za ujazo 166.65 juu ya usawa wa bahari ambayo yanatosheleza kuanza kuzalisha umeme kwani kima cha maji ambacho kinaweza kuzalisha umeme ni mita za ujazo163.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, ni kweli kuna changamoto ya umeme hivyo kipaumbele kwa sasa ni kujikita katika kupata umeme wa uhakika na wananchi wana haki ya kujua hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ili kuondoa changamoto hiyo.

Ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika mabwawa ya uzalishaji umeme, Dkt. Biteko ameelekeza TANESCO kuwa sehemu ya mkakati ya utunzaji mazingira, kwani baadhi ya watu wanachepusha mito na kuharibu mazingira hali ambayo inapelekea hadi umeme kutozalishwa wa kutosha na anayelaumiwa ni TANESCO hivyo amelitaka Shirika hilo kutenga fedha za kutosha ila kila mdau anayehusika katika usimamizi wa mazingira ahusishwe.

Pamoja na kupongeza wataalam kwa kazi nzuri ya ujenzi mradi wa JNHPP, amewataka kwenda kwa kasi zaidi kwani takriban watu milioni 63 nchini wanaitegemea TANESCO kupata umeme wa uhakika.

Vilevile, Dkt. Biteko amemtaka Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati kusimamia suala la TANESCO, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) na Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Nishati, kuja na mpango wa miaka 20 au 30 ijayo wa upatikanaji nishati kiwemo umeme kwani mahitaji yanazidi kuongezeka na Wizara ya Viwanda na Biashara ishirikishwe ili kuwa na mipango thabiti ya upatikanaji na usambazaji umeme ikiwemo kwenye viwanda ambavyo vinazidi kuongezeka.

Gharama za utekelezaji mradi wa JNHPP ni Trilioni 6.5 na Serikali imeshamlipa mkandarasi kampuni ya JV Elsewedy na Arab Contractors shilingi Trilioni 5.76 ambayo ni sawa na asilimia 87.83.