Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

VIONGOZI NENDENI MKASIKILIZE W...

VIONGOZI NENDENI MKASIKILIZE WANANCHI-DKT. DOTO BITEKO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali nchini kwenda kwenye maeneo ya wananchi kwa ajili ya kutoa huduma, kusikiliza kero zao na kuzitatua.

Amesema hayo tarehe 28 Septemba, 2023 katika Kijiji cha Nyakanazi Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera akiwa njiani kuelekea wilayani Ngara kuwasha umeme vijijini pamoja na kuhudhuria Mkutano wa Mawaziri wa Nishati kutoka nchi za Tanzania, Burundi na Rwanda wanaohusika na Mradi wa umeme wa Rusumo utakaozalisha megawati 80.

“Viongozi wenzangu tutoke maofisini na tuwafuate wananchi walipo, haina maana yoyote kama kuna kiongozi hapa na kuna shida ipo na haijawahi kutatuliwa, Mhe, Rais anachotaka ni wananchi hawa kusikilizwa na kama kuna kero sisi tuzimalize kabla yeye hajaja, wananchi wakisema kuna shida sisi tuzimalize, yeye kazi yake kubwa ni kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo.” Amesema Dkt.Biteko

Aidha, Dkt. Biteko ameendelea kusisitiza kuhusu matumizi sahihi ya fedha za Serikali ili wananchi wapate huduma stahiki na hivyo kuwapunguzia kero wanazopata wakati wakijiletea maendeleo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Doto Biteko ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupeleka umeme kwenye eneo la Kabulaishoke katika kijiji cha Nyakanazi baada ya viongozi wa eneo hilo kumweleza kuwa bado halina umeme; ambapo Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amemuahidi Naibu Waziri Mkuu kuwa, mkandarasi, kampuni ya Nakuroi ataanza kazi katika eneo hilo ndani ya mwezi mmoja.

Aidha, Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuwa na mpango maalum wa kusambaza umeme kwenye eneo hilo la Nyakanazi kutokana na kupitiwa na miundombinu ya umeme kutoka kituo kikubwa cha umeme cha Nyakanazi ambacho kinasambaza kwenye maeneo mengine ya nchi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu, amekagua kituo cha umeme cha Nyakanazi ambacho kitapokea umeme kutoka mradi wa wa umeme wa Rusumo kupitia njia ya msongo wa kV 220 na kusambaza kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.

Akiwa kituoni hapo, Dkt.Doto Biteko amezungumza na vijana wa kitanzania wanaoendelea na ujenzi wa eneo kutakapowekwa mtambo wa kupoza umeme kabla ya kuwasambazia wananchi ambapo amewaeleza vijana hao kuwa, kazi wanayofanya ni kwa ajili ya heshima ya nchi kwani umeme kutoka kituo hicho utahudumia wananchi.

Ameongeza kuwa, Serikali inathamini nguvu kazi wanayotumia kwani umeme kutoka kituo hicho utaenda kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Biharamulo, Geita ,Shinyanga na Kigoma ili kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.