WAANDAAJI WA MAUDHUI KUWEZESHWA KUNUFAIKA KIUCHUMI KUPITIA UHAMASISHAJI WA NISHATI SAFI.
Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, ameshiriki mafunzo maalum kwa waandaaji wa maudhui (content creators) yaliyofanyika Machi 25,2026, mkoani Dar es Salaam yakilenga kuwajengea uwezo ili kuboresha ubunifu na kuongeza tija ya kazi zao.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, huku Wizara ya Nishati ikiwa miongoni mwa wawezeshaji wakuu.
Kupitia mafunzo hayo washiriki watapatiwa elimu kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo kwa waandaaji wa maudhui kupitia uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Namna Waandaaji wa maudhui wataweza kujipatia kipato kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazohusika na nishati safi, kushiriki kampeni za udhamini, matangazo ya bidhaa na huduma zinazohusiana na nishati safi pamoja na kutengeneza maudhui ya kielimu yanayovutia hadhira.
Kupitia ubunifu wao, wanaweza kuvutia wadau na wafadhili hivyo kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.
Ushiriki wa Wizara ya Nishati katika mafunzo hayo unaonesha kutambua mchango mkubwa wa waandaaji wa maudhui kama daraja muhimu la kufikisha elimu kwa umma na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia majukwaa yao ya kidijitali