The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

Wachoma Nyama Dodoma Waanza Ku...

Wachoma Nyama Dodoma Waanza Kuhamia Matumizi Ya Majiko Ya Gesi

Wizara ya Nishati kupitia Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia imefanya ziara ya kutembelea mjasiriamali anayejishughulisha na uchomaji wa nyama katika eneo la Maili Mbili, jijini Dodoma ili kujionea namna anavyonufaika na matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia majiko ya gesi.

Akizungumza katika ziara hiyo Machi 6, 2026, Mjasiriamali huyo, Bw. Mathias Leganga, amesema mwitikio wa wateja umeongezeka tangu aanze kutumia jiko la gesi kuchoma nyama.

Amesema wateja wengi wamevutiwa na ubora wa nyama inayochomwa kwa kutumia gesi, akieleza kuwa huiva vizuri bila kupoteza radha yake, tofauti na ilivyokuwa wakati alipokuwa akitumia majiko ya mkaa na kuni hapo awali.

“Kuna mwitikio mkubwa wa wateja kwa sababu nyama inakuwa safi, inaiva vizuri na haipotezi ladha yake kama ilivyokuwa wakati natumia mkaa na kuni,” amesema Leganga.

Ameeleza kuwa alianza biashara ya uchomaji wa nyama mwaka 2005 akitumia nishati ya mkaa na kuni, lakini baada ya kupata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, sasa ameanza kutumia jiko la gesi kwa takribani wiki tatu.

Kwa sasa, amesema huchoma mbuzi kati ya wawili hadi watatu kwa siku, huku akibainisha kuwa jiko la gesi limeongeza ufanisi wa kazi kwani halichoshi, linaokoa muda na linazingatia usafi wakati wa uchomaji wa nyama.

Aidha, Leganga ameomba Serikali na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili watu wengi zaidi waweze kuhamia kwenye matumizi hayo.

“Ningependa kuona wachoma nyama wengine kutoka maeneo mbalimbali nchini wanahamia kwenye nishati safi kwa sababu gharama zake ni nafuu ukilinganisha na ununuzi wa mkaa,” amesema.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi. Benezeti Kabunduguru, amesema serikali itaendelea kuhamasisha wachoma nyama na wajasiriamali wengine kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa kuni na mkaa pamoja na kulinda mazingira.

“Tutendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wachoma nyama na wananchi kwa ujumla. Pia tunawakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana nasi katika kuendeleza kampeni hizi ili kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanaongezeka nchini,” amesema Mha. Kabunduguru.