WADAU WA TEKNOLOJIA ZA NISHATI SAFI YA KUPIKIA WATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU
Wadau wa uzalishaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia wametakiwa kuongeza ubunifu katika bidhaa zao ili ziweze kumudu gharama kwa wananchi wengi zaidi sambamba na kupanua upatikanaji wake kote nchini.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa agizo la Ofisi ya Makamu wa Rais linalozitaka taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia, jijini Arusha.
Katika ziara hiyo, Mlay ametembelea na kufanya mazungumzo na waendelezaji pamoja na wasambazaji wa teknolojia na bidhaa za nishati safi ya kupikia, zikiwemo Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Kampuni ya Godil Metal Works na Gilsun Technology.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mlay amesema SIDO imekuwa mstari wa mbele katika kutengeneza majiko ya nishati safi ya kupikia kwa ajili ya taasisi na kaya, huku ikihakikisha bidhaa hizo zinapatikana kwa wananchi.
“SIDO wanatengeneza majiko mbalimbali ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi na kaya. Wanafanya kazi kubwa kuhakikisha majiko haya yanapatikana, hivyo wabunifu wengine nao wahamasike kubuni bidhaa zenye gharama nafuu ili mtumiaji aweze kuzimudu,” amesema Mlay.
Aidha, amesema agenda ya nishati safi ya kupikia ni kipaumbele cha Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo Wizara ya Nishati ina jukumu la kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa ipasavyo.
Amefafanua kuwa lengo la Serikali ni kufikisha asilimia 80 ya Watanzania katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, akisisitiza kuwa taasisi zote zina wajibu wa kushirikiana ili kufanikisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi.
“Ni jukumu la kila taasisi kuhakikisha Watanzania wanahama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia,” amesisitiza.
Kadhalika, Mlay amezitaka taasisi ambazo tayari zimewekeza katika miundombinu ya nishati safi ya kupikia kuendelea kuitumia kikamilifu, badala ya kurejea katika matumizi ya nishati isiyo safi, hali ambayo inakinzana na juhudi za Serikali katika kulinda afya za wananchi na mazingira.