WADAU WAJADILIANA MBINU ZA KUFIKIA WALENGWA ILI KUFANIKISHA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Wadau wa masuala ya Nishati safi ya kupikia zikiwepo Wizara na Taasisi mbalimbali nchini, wamekutana Jijini Dodoma na kujadili mbinu mbalimbali za kufikia wadau muhimu zitakazowezesha kufikisha asilimia 80 ya wananchi wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.
Mbinu zilizojadiliwa ni pamoja na upelekaji wa elimu ya Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia kwa Wananchi kupitia majukwaa na shughuli mbalimbali za Kijamii zikiwemo Mbio za Mwenge wa Huru pamoja na Siku ya mwanamke duniani, lengo likiwa kupitia kaulimbiu wananchi wanapata elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mhandisi kutoka Wizara ya Nishati Bi. Anita Ringia amesema kwamba “upo umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakiwemo vijana na watafiti ili kubuni suluhisho kupitia tafiti zao zinazoweza kusaidia kukuza maendeleo ya nishati safi ya kupikia badala ya tafiti hizo kuwekwa kabatini bila kutumika” amesema Ringia. Aliongeza kuwa litengenezwe jukwaa la kuwakutanisha watafiti na watekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ili kupata suluhisho zinazohitajika kwa wakati sahihi” Amesema Ringia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya ushauri na usimamizi wa biashara (Kengo Limited), Bi. Sarah Majengo amesema lengo la kukutanisha wadau wa masuala ya Nishati safi ya kupikia ni kutambua wadau muhimu katika utekelezaji, majukumu yao, namna ya kuwafikia pamoja na kuendelea kukusanya maoni mbalimbali ambayo yatasaidia kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia sambamba na kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Wananchi.
“Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni agenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali, umuhimu wa agenda hii unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi” amesema Majengo.
Ameeleza kuwa, ushirikishwaji wa wadau utasaidia ujumbe wa nishati safi ya kupikia kufika kwa watu sahihi, kwa kuzingatia jinsia, majukumu ya kijamii pia utumiaji wa lugha ambayo inaeleweka kwa kila mwananchi.
