The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

WAJASIRIAMALI NA BODABODA WAFI...

WAJASIRIAMALI NA BODABODA WAFIKIWA NA ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA MOROGORO

Wajasiriamali na bodaboda katika Soko Kuu la Kingalu, Stendi Kuu ya Mabasi Msamvu na maeneo ya Kihonda mkoani Morogoro wamepatiwa elimu ya nishati safi ya kupikia kupitia kampeni inayoendelea nchini yenye lengo la kuhamasisha mabadiliko ya tabia kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Timu kutoka Wizara ya Nishati na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF), tarehe 25 Februari 2026 ilizungumza na wajasiriamali na waendesha bodaboda ili kubaini aina ya nishati wanazotumia na kuwapatia elimu juu ya umuhimu wa kuhamia katika nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi na umeme.

Baadhi ya wananchi, akiwemo Bwana Juma Tengeni mjasiriamali wa Stendi ya Msamvu, wameeleza kuwa wanapenda kutumia gesi na umeme lakini wanaomba gharama bado ziwe rafiki, pamoja na kuongeza elimu kuhusu matumizi sahihi ya majiko ya umeme.

Katika kampeni hiyo, wananchi wameoneshwa namna majiko ya gesi na umeme yanavyopika kwa haraka na gharama nafuu na hivyo kuongeza mwitikio wa kuhamia katika nishati safi ya kupikia.