The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

WARSHA YA MOROGORO YALENGA KUI...

WARSHA YA MOROGORO YALENGA KUIMARISHA USHIRIKIANO KWA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

Mshauri wa Mawasiliano kutoka Kampuni ya Kengo, Bi. Niwaeli Gittens-Mbaga, ameendesha mada kuhusu nafasi ya vyombo vya habari kama wadau muhimu katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akieleza umuhimu wa kujenga mahusiano imara na wadau mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa ajenda hiyo.

Mafunzo hayo yametolewa katika siku ya pili ya warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa Habari na maafisa mawasiliano Serikalini wa Mikoa, Wizara na Taasisi kuhusu uandishi na uhamasishaji wa masuala ya nishati safi ya kupikia yanayoendelea mkoani Morogoro.

Katika uwasilishaji wake, Bi. Gittens - Mbaga aliwaelekeza washiriki kuhusu mbinu za kuwasiliana na wadau wa nishati safi ya kupikia, namna ya kuandaa na kuwasilisha maombi pamoja na mapendekezo ya miradi (proposals), huku wakizingatia maslahi na vipaumbele vya kila mdau ili kuongeza uwezekano wa kupata ushirikiano na rasilimali.

Baada ya kumaliza mada hiyo, washiriki waligawanywa katika makundi kwa ajili ya kufanya mazoezi ya vitendo (practical), ambapo kila kundi lilipewa jukumu la kuandaa na kuwasilisha pendekezo la mradi wa nishati safi ya kupikia kwa kuzingatia maarifa waliyopata wakati wa mafunzo.

Makundi hayo yaliwasilisha mada na mapendekezo yao mbele ya washiriki wenzao na wawezeshaji, hatua iliyotoa fursa ya kupata mrejesho na kuboresha uelewa wa namna bora ya kushirikiana na wadau katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mikakati ya mawasiliano yenye tija.