The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

WATANZANIA MILIONI MOJA KUNUFA...

WATANZANIA MILIONI MOJA KUNUFAIKA NA MIKOPO YA MAJIKO YA UMEME KUPITIA TANESCO.

Watanzania milioni moja wanatarajiwa kunufaika na mpango wa mikopo ya majiko ya umeme kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kufuatia utiaji saini wa makubaliano kati ya shirika hilo na wadau wa uzalishaji na usambazaji wa vifaa vya nishati safi ya kupikia vinavyotumia umeme.

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo leo Juni 11, 2026, katika Viwanja vya Mashujaa Jamatini jijini Dodoma.

Kupitia makubaliano hayo, TANESCO inatarajia kuwawezesha wateja wake wapya na wale waliokwishaunganishiwa umeme kupata majiko ya umeme kwa mkopo, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini na kuondoa changamoto ya gharama za awali za ununuzi wa majiko hayo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema mikopo hiyo itatolewa kwa wateja wote wa zamani na wapya wa shirika hilo watakaokidhi vigezo vilivyowekwa.

Amevitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na mwombaji kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA), kuwa mteja wa TANESCO kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu, pamoja na kuwa mmiliki wa kaya.

Twange amesema marejesho ya mikopo hiyo yatafanyika kupitia manunuzi ya umeme ya wateja watakaonufaika na mpango huo, huku muda wa kurejesha mkopo ukiwa kati ya miezi mitatu hadi sita kulingana na makubaliano husika.

Aidha, amesema makubaliano kati ya TANESCO na wadau hao yatatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu, huku yakitarajiwa kuongeza upatikanaji wa majiko ya umeme kwa wananchi na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.