“WATEJA WA TANESCO WAHUDUMIWE KWA HARAKA NA BILA URASIMU” MHE. SALOME.
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, ameitaka TANESCO kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wateja zina viwango vinavyofanana katika mikoa yote nchini bila kujali eneo husika kwani hatua hiyo itasaidia kupunguza mkanganyiko kwa wananchi pamoja na kuongeza uaminifu kwa Shirika hilo.
Akifungua mkutano wa mwaka wa Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO unaofanyika mkoani Dodoma leo Mei 18, 2026 Mhe. Salome amesema bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo kuchelewa kutatuliwa kwa hitilafu za umeme, kufungwa kwa tiketi kabla huduma haijakamilika pamoja na ucheleweshaji wa taarifa kuhusu kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo.
Ameongeza kuwa mteja anatakiwa kuwa kipaumbele katika kila hatua ya utoaji huduma na kwamba watumishi wote wanapaswa kutoa huduma kwa haraka, kwa heshima na kwa ufanisi bila urasimu usio wa lazima.
Aidha, amewataka watumishi wa idara za ufundi kuhakikisha tiketi hazifungwi kabla changamoto za wananchi hazijatatuliwa kikamilifu.
Kwa upande mwingine, amewataka wataalamu hao kuwa makini wanapounganisha tiketi za changamoto mbalimbali ili kuepusha usumbufu kwa wateja kwani kuunganisha tiketi zisizohusiana husababisha malalamiko zaidi na kuathiri taswira ya Shirika mbele ya wananchi.
Mhe. Salome amehitimisha kwa kuwataka watumishi wa TANESCO kuwa balozi wema wa Shirika hilo na kuzingatia viwango bora vya huduma kwa lengo la kujenga taswira chanya kwa wananchi.