Watumishi Wapongeza Utekelezaji wa Mradi wa EACOP Kwa Kuzingatia Uhifadhi wa Mazingira
Watumishi wa Wizara ya Nishati wameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). wakieleza kuwa katika hatua zote za utekelezaji, mradi umezingatia kwa kina masuala ya uhifadhi wa mazingira na viumbe hai katika maeneo yote yanayopitiwa.
Kauli hiyo imetolewa Februari 22, 2026, Chongoleani, Tanga Mkuu wa safari hii Benson Lukuta wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo iliyofanywa na watumishi kutoka Wizara ya Nishati, akiwa Mkuu wa Msafara.
Ziara hiyo ililenga kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa, hususan jinsi unavyozingatia uhifadhi wa mazingira na ulinzi wa viumbe hai katika maeneo yanayopitiwa na bomba.
“Utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati umezingatia taratibu zote za uhifadhi wa mazingira. Mradi huu unaunganisha Tanzania na Uganda na ni mojawapo ya miradi mikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, ukiwa na lengo la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania,” alisema Lukuta.
Kwa upande wake, Bw. Thomas De Mauleon kutoka kampuni ya CSR alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa Watanzania, si tu kiuchumi bali pia kijamii na kitaalamu.
Aidha, amesema mradi umeweza kutoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 9,194, huku wananchi 170 wakipatiwa mafunzo maalum ili kufikia viwango vya kimataifa katika ujenzi wa miradi ya mafuta na gesi.
Pia, kupitia miradi ya kijamii, EACOP imeboresha barabara na huduma za maji katika maeneo yanayopakana na mradi. Takribani kilomita 27 za barabara za changarawe zimeboreshwa, zikiwemo:Barabara ya Kagongwa hadi Sojo (km 18), Handeni kuelekea Kambi Na. 15 (km 2.1), Handeni kuelekea Chongoleani (km 7.2).
Hatua hizi zinaongeza urahisi wa usafirishaji, kuunganisha jamii na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo yanayopitiwa na mradi.