Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

WAZALISHAJI WADOGO WA UMEME WA...

WAZALISHAJI WADOGO WA UMEME WAPATA TUMAINI JIPYA

Waishukuru Serikali kwa uwezeshaji

Serikali yaahidi kuendelea kutatua changamoto zao

Dkt. Biteko awataka kujiamini, Serikali inawathamini

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Wazalishaji wadogo wa umeme ambapo amewaeleza kuwa, Serikali inawatambua na kuthamini mchango wao katika uchumi, hivyo wanapaswa kujiamini na kuendelea kubuni miradi mipya ya kuzalisha umeme ili nchi ipate umeme wa kutosha.

Dkt. Biteko alisema hayo tarehe 21 Februari 2024 wilayani Njombe mkoani Njombe katika kikao chake na Wazalishaji Wadogo wa umeme ambacho pamoja na mambo mengine, wazalishaji hao walieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa kazi zao pamoja na njia za kuendeleza miradi hiyo.

“Nataka mtambue kuwa, Serikali haitegemei umeme kutoka vyanzo vikubwa tu kama vile Gesi au mradi wa Julius Nyerere, bali dhamira yetu ni kuendeleza vyanzo vingine ikiwemo hivi vidogo vya umeme, hata kama chanzo kinazalisha kilowati moja sisi tunakithamini, hivyo mnapaswa kujiamini kwani mchango wenu ni mkubwa kwenye Sekta hii.” Alisema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko aliwapongeza wazalishaji hao wadogo wa umeme kwa ubunifu wao ambao unasaidia katika kusambaza umeme kwenye maeneo ambayo gridi ya Taifa bado haijafika pamoja na kuongeza kiwango cha umeme kwenye gridi hiyo kwani wazalishaji wengine wanaiuzia TANESCO umeme ambao unaingizwa kwenye gridi.

Aliwataka kutoogopa changamoto na kwamba Serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwapatia nyenzo zinazohitajika.

Ili kutatua changamoto mbalimbali zilizotajwa na wazalishaji hao wadogo wa umeme ikiwemo suala la upatikanaji wa vibali na msamaha wa kodi kwa baadhi ya vifaa vinavyotoka nje ya nchi, Dkt. Biteko ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuandaa andiko litakaloainisha changamoto hizo ili ziweze kufanyiwa kazi na Serikali kwani Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka biashara ya umeme kuwa rahisi ili nchi iwe na nishati ya kutosha.

Kwa nyakati tofauti, wazalishaji hao wadogo wameishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono kwenye kazi zao kupitia TANESCO na REA ambao wanawawezesha kwa namna mbalimbali ikiwemo ushauri wa kitaalam, fedha na vifaa ambavyo vimewawezesha kuanza kutekeleza miradi hiyo.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria kikao hicho ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Wabunge wa Mkoa wa Njombe, Wakuu wa Wilaya na Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo.