Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Waziri Makamba akutana na uju...

​Waziri Makamba akutana na ujumbe wa Benki ya Dunia, wajadili maendeleo Sekta ya Nishati

Waziri Makamba akutana na ujumbe wa Benki ya Dunia, wajadili maendeleo Sekta ya Nishati

Na Zuena Msuya DSM,

Waziri wa Nishati January Makamba amekutana na ujumbe wa Benki ya Dunia (WB) ukiongozwa na Mkurugenzi Mkazi wa benki hiyo kwa upande wa Tanzania, Mara Warwick, na kuzungumzia mambo mbalimbali kubwa likiwa ni uendelezaji wa Sekta Nishati ikiwemo masuala ya umeme na gesi.

Katika mazungumzo hayo, Makamba ameishukuru benki hiyo kwa ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania pia kuwezesha utekelezaji wa miradi ya Maendeleo nchini ukiwemo ule wa Umeme wa kuunganisha Tanzania na Zambia (TAZA).

Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati zilizopo mkoani Dar es Salaam, Machi 28, 2022. Pamoja na mambo mengine mazungumzo hayo yamelenga zaidi kuimarisha ushirikiano kati ya benki hiyo na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Serikali ya Tanzania inaishukuru Benki ya Dunia kwa kuwezesha miradi ya nishati hapa nchini, tunawaahidi tutaendelea kushirikiana nanyi katika nyanja mbalimbali kwa kuwa tumeona matokeo chanya katika miradi ambayo benki hii imeiunga mkono hasa katika Sekta ya Nishati. " Amesema Makamba.

Mkutano huo umehudhuriwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Seif Said na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Anitha Ishengoma pamoja na Viongozi wengine waandamizi kutoka wizarani, REA na TANESCO.

Kikao hicho kimejadili mradi wa Usambazaji wa umeme vijijinj, njia kuu za kusafirisha umeme pamoja masuala ya gesi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa WB nchini Tanzania, Warwick amemueleza Waziri wa Nishati kuwa wataendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kwa kuiunga mkono Sekta ya Nishati, ili kutanua wigo wa ukuaji ya sekta hiyo.

Ameongeza kuwa, watawajengea uwezo wataalam katika Sekta ya Nishati ili kuweza kuongeza tija na ufanisi katika sekta hiyo.