Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Waziri Makamba akutana na Waz...

​Waziri Makamba akutana na Waziri wa Nishati na Madini wa Algeria

Waziri Makamba akutana na Waziri wa Nishati na Madini wa Algeria

Algiers, Algeria

Waziri wa Nishati, January Makamba tarehe 28 Oktoba 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati na Madini wa Algeria, Mohamed Arkab.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Makamba alieleza mahusiano ya kihistoria yaliyopo baina ya Tanzania na Algeria na kueleza nia ya Serikali ya Tanzania kuendeleza mahusiano hayo katika nyanja ya uchumi kwa mustakabali wa nchi hizi mbili .

Akiongea katika kikao hicho, Waziri Makamba alisema “Tanzania na Algeria tumekuwa na mahusiano ambayo ni ya kihistoria na sasa Serikali ya Tanzania ingependa kuona mahusiano ya nchi zetu mbili yanaboreshwa zaidi kwa kuwa na mahusiano ya kiuchumi ambapo kwa kuanzia tunaangalia sekta ya nishati ambayo wenzetu Algeria mmepiga hatua kubwa”.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini wa Algeria, Mohamed Arkab alieleza utayari uliopo ndani ya Serikali ya Algeria kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Waziri Arkab alisema “Kwanza tunafurahi sana kwa Serikali ya Tanzania kutaka kukuza mahusiano yetu zaidi na hususan katika eneo la kiuchumi ambalo ni kweli tuna nafasi ya kuboresha zaidi kwa manufaa ya nchi zetu mbili”.

Waziri Arkab alifafanua zaidi kuwa, Algeria ina uzoefu mkubwa katika eneo la nishati ikijumuisha mafuta na gesi ambapo wanazalisha mafuta na gesi na kuuza ndani na nje ya Algeria na wateja wakubwa ni nchi za Ulaya kwa kuwa kijiografia wako karibu zaidi. “kupitia kampuni ya Taifa ya Mafuta, Sonatrach na kampuni zake tanzu, tumeweza kujenga mtandao wa takribani kilometa 22,000 wa kusambaza gesi ndani ya nchi pamoja na bandari za kupakia mafuta katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi” alisema Wazri Arkab.

katika ziara hiyo Waziri Makamba aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio na Kamishna wa Petroli na Gesi, Michael Mjinja.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alieleza fursa zilizopo katika mkondo wa juu na chini wa sekta ya mafuta na gesi nchini ambapo aliwakaribisha Algeria kuwekeza na kushirikiana na TPDC katika maeneo hayo.

Tanzania imeingia katika uchumi wa kati ambapo mahitaji ya nishati ndani ya nchi yameongezeka na hivyo uwekezaji zaidi katika kusambaza gesi asilia ni muhimu na pia kuhakikisha tunaendelea kufanya shughuli za utafutaji ili kuendana na mahitaji yanayokuwa siku hadi siku, hivyo tunaamini ushirikiano baina ya nchi zetu ni muhimu kwa mustakabali wa nchi zetu” alieleza Dkt. Mataragio

Kwa upande wake Kamishna wa Petroli na Gesi, Ndg. Michael Mjinja alieleza uhitaji mkubwa wa nishati uliopo Tanzania na kusisitiza kuwa Algeria wanakaribishwa kwa mikono miwili kuwekeza nchini Tanzania.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Sonatrach, Toufik Hakkar, Mkurugenzi Mkuu wa Sonelgaz, Chahar Boulakhras na maafisa waandamizi wengine kutoka Serikali ya Algeria pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Algeria Balozi Meja Jenerali Jacob Gideon Kingu, Mwambata wa Jeshi, Brigedia Jenerali Adolf Peter Mutta na maafisa wengine kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria.