Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​WAZIRI MAKAMBA AZINDUA KIWAND...

​WAZIRI MAKAMBA AZINDUA KIWANDA CHA TRANSFOMA

WAZIRI MAKAMBA AZINDUA KIWANDA CHA TRANSFOMA

Waziri wa Nishati, January Makamba, Septemba 12, 2022 amezindua kiwanda cha kuzalisha transfoma ikiwa ni awamu ya pili ya kiwanda cha kuzalisha vifaa vya umeme cha Elsewedy Electrica Industrial Complex kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Awamu ya kwanza ya kiwanda hicho inayohusisha utengenezaji wa nyaya za umeme ilizinduliwa Desemba 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan.

Awamu ya pili ya kiwanda hicho ambayo inahusisha uzalishaji wa transfoma itawezesha kiwanda kuwa na uwezo wa kuzalisha trasfoma 2,500 kwa mwaka na kikitarajiwa kutengeneza ajira 1500.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Waziri Makamba amepongeza uwekezaji huo na kueleza Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji.

“Ni mafanikio makubwa kuona awamu ya pili ya kiwanda inakuja ikiwa ni miezi sita tu tangu kuanza kwa uzalishaji wa awamu ya kwanza,” amesema

“Hii inaonyesha kiasi gani mmedhamiria kufanya uwekezaji wenye tija. Upande wetu Serikali tutaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa biashara,” amesema Makamba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Elsewedy Electric East Africa, Ibrahim Qamar amesema uzalishaji huo wa transoma 2500 kwa mwaka unaweza kuongezeka kulingana na uhitaji katika soko.

“Uzinduzi wa kiwanda cha transfoma unazidi kufungua milango ya ushirikiano kati ya Tanzania na Misri. Kiwanda hiki kitasaidia kuingiza utalaam huu hapa Tanzania na kuwajengea uwezo watalaam wa hapa nchini,” amesema

“Ahadi yetu ni kwamba tutendelea kuzitafuta na kuziendeleza fursa ambazo zinaunga mkono mpango mkakati wa kuendeleza viwanda nchini Tanzania,” amesema Qamar.

Kiwanda hicho kilichojengwa na kampuni ya wazawa ya Advent Construction Limited kinatarajia pia kupanua uzalishaji wake wa nyaya na transfoma sambamba na kuanzisha uzalishaji wa mita na PVC.