The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

WAZIRI NDEJEMBI AAGIZA UKARABA...

WAZIRI NDEJEMBI AAGIZA UKARABATI WA KITUO CHA KUFUA UMEME HALE UKAMILIKE JULAI 31, 2026.

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius J. Ndejembi amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi wa ukarabati wa Kituo cha Kufua Umeme Hale kukamilisha kazi ifikapo Julai 31, 2026, akieleza kuwa Serikali haitaongeza muda wa ziada iwapo atashindwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Ametoa agizo hilo tarehe Juni 29, 2026 wakati akikagua maendeleo ya ukarabati mkubwa wa Kituo cha Kufua Umeme Hale kilichopo mkoani Tanga katika Bonde la Mto Pangani kilichozinduliwa mwaka 1964. Ukarabati huo unalenga kurejesha ufanisi wa kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha megawati 21.

Amesema Serikali itachukua hatua za kimkataba dhidi ya Mkandarasi iwapo atashindwa kukamilisha kazi hiyo, ikizingatiwa kuwa mradi huo ulipaswa kukamilika miezi 10 iliyopita, lakini TANESCO ilifanya tathmini na kumwongezea muda Mkandarasi.

“Mkataba wake unakamilika Julai 31, 2026. Nimemuelekeza Mkandarasi kuwa hatutamuongezea muda mwingine, kwani tulishamuongezea muda ili aweze kukamilisha kazi. Cha kuridhisha ni kwamba asilimia 94 ya vifaa vyote vinavyohitajika kukamilisha mradi huu vipo hapa site”. Amesema Ndejembi.

Amesema mradi huo ukikamilika utawezesha kuzalishwa kwa megawati 21 ambazo zitaingizwa kwenye Gridi ya Taifa ya Umeme, hatua itakayoongeza upatikanaji wa umeme katika mikoa ya kaskazini, hususan Mkoa wa Tanga ambako mahitaji ya umeme yanaendelea kuongezeka.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa umeme ni hitaji la msingi kwa wananchi katika utoaji wa huduma mbalimbali, ndiyo maana Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi ili kuhakikisha kunakuwa na umeme wa kutosha kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania.

Ameeleza kuwa ukarabati wa kituo hicho unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Sweden kupitia SIDA, kwa gharama ya shilingi bilioni 64 (dola za Marekani milioni 24.81).

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANESCO, Mha. Timothy Mugaya amesema kazi ya ukarabati wa miundombinu ya Kituo cha Kufua Umeme Hale imefikia asilimia 83.3.

Mha. Timothy amesema TANESCO itaendelea kumsimamia Mkandarasi, Dongfang Electric International Corporation kutoka China, kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili aweze kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliowekwa kwa mujibu wa mkataba.

Ukarabati wa kituo hicho unahusisha ujenzi wa kituo kipya cha kupozea umeme, uboreshaji wa mfumo wa kuendesha mitambo, usimikaji wa mitambo mipya ya kuzalisha umeme, uimarishaji wa handaki la kuingiza na kutoa maji kwenye mitambo, pamoja na ukarabati wa miundombinu ya bwawa.