WAZIRI NDEJEMBI APOKEA TAARIFA YA TATHMINI MRADI WA MALAGARASI.
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, leo Juni 10, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na timu ya wakaguzi wa Mradi wa Malagarasi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa lengo la kupokea taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, na kuhudhuriwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Bw. Petro Lyatuu, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, pamoja na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.
Ikumbukwe kwamba Mei 10, 2026 Waziri Ndejembi alifanya ziara katika mradi wa umeme wa Malagarasi mkoani Kigoma na kueleza kutoridhishwa kwake na mwenendo wa utekelezaji wa Mradi huo wa megawati 49.5 katika maporomoko ya Mto Malagarasi.
Hiyo ni kutokana na kuchelewa kwa kazi pamoja na kutotekeleza masharti ya mkataba ambayo kampuni ya Dongfang ya China iliingia na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Kutokana na hilo aliielekeza TANESCO kufanya ukaguzi wa mradi na kuwasilisha taarifa ofisini kwake.