Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

Waziri wa Nishati afanya mazun...

Waziri wa Nishati afanya mazungumzo na Balozi wa Marekani na Uholanzi

Waziri wa Nishati afanya mazungumzo na Balozi wa Marekani na Uholanzi

Ataja vipaumbele

Waziri wa Nishati, January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald J.Wright pamoja na Balozi wa Uholanzi, Wiebe De Boer ambapo alitaja vipaumbele katika Sekta ya Nishati.

Mazungumzo yake na Mabalozi hao yalifanyika tarehe 8 Oktoba, 2021 katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati zilizopo mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watendaji mbalimbali akiwemo Kamishna wa Umeme na Nishati na Jadidifu, Felchesmi Mramba, Kamishna wa Petroli na Gesi, Michael Mjinja, na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio.

Katika kikao chake na Balozi wa Marekani, Waziri Makamba alimueleza Balozi huyo vipaumbele mbalimbali vya Serikali katika Sekta ya Nishati ikiwemo upatikanaji wa umeme hasa katika maeneo ya vijijini, kwani Serikali imefanya kazi kubwa ya kupeleka umeme maeneo hayo lakini wananchi wengi bado wanahitaji huduma hiyo.

Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni uwepo wa nishati endelevu za kupikia mfano gesi ya kwenye mitungi (LPG) ambayo itawafanya wananchi wengi waache kutumia mkaa na kuni kwa kupikia na hivyo kuondoa suala la uharibifu wa misitu ambalo pia linapelekea mabadiliko ya tabia nchi.

“Kipaumbele kingine, ni kuzifanya Taasisi zilizo chini ya Wizara kama vile TANESCO, TPDC na EWURA, kuwa na uwezo wa RasiliMali Watu pamoja na uwezo wa kifedha utakaoziwezesha Taasisi hizo kuwa na ufanisi pamoja na usimamizi madhubuti wa Sekta ya Nishati hasa katika kipindi ambacho Tanzania inaenda kuwa nchi yenye umeme wa kutosha katika ukanda huu.” Alisema Makamba

Kwa upande wake Balozi wa Marekani, Donald J. Wright, alisema ataendelea kufanya kazi na Wizara na kwamba kumekuwa na ushirikiano wa takriban miaka 60 kati ya Tanzania na nchi hiyo na eneo mojawapo la ushirikiano huo ni sekta ya Nishati.

Katika mazungumzo yake na Balozi wa Uholanzi nchini, Wiebe De Boer, Waziri wa Nishati alitaja maeneo mbalimbali yanayohitaji ushirikiano, kubwa ikiwa ni kupeleka umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme wa gridi kama vile visiwa kwa kuweka mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo Jua ambalo linapatikana katika maeneo yote ya Tanzania.

Aliishukuru Uholanzi kwa kuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania kwa miaka mingi na kwamba ushirikiano wa nchi hizo mbili upo katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati.

Balozi wa Uholanzi, Wiebe De Boer alimweleza Waziri wa Nishati kuwa, Serikali isisite kuwasiliana na Ubalozi huo pale inapoona kuna uhitaji wa kuungwa mkono mkono katika utekelezaji wa mipango mbalimbali.