Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Wizara ya Nishati yaahidi ush...

​Wizara ya Nishati yaahidi ushirikiano kwa watengenezaji wa magari ya umeme

Wizara ya Nishati yaahidi ushirikiano kwa watengenezaji wa magari ya umeme

Na Teresia Mhagama, Arusha

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, amesema kuwa, Wizara ya Nishati itatoa ushirikiano kwa wabunifu pamoja na kampuni zinazotengeza magari yanayotumia umeme ili kuwezesha wananchi kuwa na vyanzo mbalimbali vya kuendesha magari badala ya kutegemea mafuta kama chanzo kikuu.

Alisema hayo tarehe 06 Juni, 2022 mkoani Arusha, wakati alipofanya ziara katika Shule ya Sayansi Arusha pamoja na kampuni ya kitanzania inayotengeneza magari ya umeme ya Hanspaul Group ili kuona ubunifu na pia kufahamu kama kuna changamoto zozote zinazohitaji utatuzi kutoka serikalini.

Akiwa katika Shule ya Sayansi Arusha, alielezwa na Mkuu wa Shule hiyo, Mary Mbise, kuwa, shule hiyo inafundisha Sayansi na Teknolojia kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita, ambapo wanafunzi hao wanapata nafasi ya kufanya ubunifu ili kuweza kusaidia jamii mara baada ya kuhitimu.

Akiwa katika shule hiyo, Naibu Katibu Mkuu, alishuhudia ubunifu wa gari linalotembea kwa kutumia nishati ya umeme jua, printer ya 3D pamoja na jokofu linalotumia nishati hiyo ambalo lengo lake ni kuwasaidia wajasiriliamali wadogo wadogo hasa wanaouza mboga za majani ambapo badala ya mboga hizo kuzinyunyizia maji ili zisinyauke, zinawekwa kwenye jokofu hilo linaloitwa solar cooler house.

Naibu Katibu Mkuu aliwapongeza wanafunzi pamoja uongozi wa Shule hiyo kwa ubunifu wao na kueleza kuwa Wizara ya Nishati itawapa ushirikiano ikiwamo kuangalia fursa za kuongeza ujuzi kupitia miradi mbalimbali na uwekezaji.

Akiwa katika kampuni ya Hanspaul, Naibu Katibu Mkuu alishuhudia jinsi magari yanayotumia umeme yanavyotengenezwa ambapo alielezwa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Satbir Hanspaul kuwa, magari hayo kwa sasa yameanza kutumika katika shughuli za utalii ambapo yanapeleka watalii katika mbuga mbalimbali ikiwemo Serengeti.

Hanspaul alisema magari hayo yameanza kutumika katika Sekta ya Utalii ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye amezidi kufungua fursa katika Sekta ya Utalii wa Tanzania kupitia Filamu ya Royal Tour.

Aliongeza kuwa, kampuni hiyo imeona fursa na kutengeneza magari yanayotumia umeme kwenda kwenye Mbuga za Wanyama ambapo magari hayo hayana uchafuzi wa mazingira, hayatoi kelele yanapokuwa mbugani na pia gharama zake za uendeshaji ni nafuu.

Hanspaul, alimshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa kufanya ziara katika kampuni hiyo kwanibaada ya kuzungumza na watendaji wa kampuni hiyo ametoa muongozo ili teknolojia inayofanyika kiwandani hapo iwasaidie watanzania wengi zaidi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe.Mrisho Gambo alimpongeza Naibu Katibu Mkuu na ujumbe wake kwa kutembelea kiwanda hicho ili kufahamu masuala mbalimbali ikiwemo changamoto wanazopata na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi na kueleza kuwa, suala hilo linawafanya wadau mbalimbali wajenge imani zaidi kwa Serikali ya Awamu ya Sita.

Baada ya ziara kiwandani hapo, Naibu Katibu Mkuu aliwapongeza watendaji wa kampuni hiyo kwa teknolojia hiyo inayofanyika nchini Tanzania ambayo imetoa ajira kwa vijana wa kitanzania na kwamba changamoto mbalimbali zilizoelezwa na kampuni hiyo zitafanyiwa kazi na Serikali.

Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu aliambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Mrisho Gambo, Mkurugenzi wa Umeme kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Eng. Godfrey Chibulunje, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Eng.Herini Mhina, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Eng.Barozi Patrick na Wataalam wengine kutoka EWURA na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).