WIZARA YA NISHATI YAPEWA KONGOLE NA KAMATI YA BUNGE KWA UBUNIFU WA MIRADI YA NISHATI
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali inayorahisisha upatikanaji wa huduma za nishati kwa wananchi.
Mhe. Mgalu ametoa pongezi hizo tarehe 12 Februari 2026 jijini Dodoma wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Wizara ya Nishati kwa Kamati hiyo kuhusu mipango, uwekezaji na ufuatiliaji wa miradi ya nishati nchini.
“Kupitia taasisi zenu, mmekuwa mkibuni miradi mbalimbali ambayo tumeona ikileta tija kwa wananchi. Mfano ni miradi ya ujazilizi wa umeme vijijini ambayo ililenga kusambaza umeme katika maeneo ambayo miundombinu ilikuwa imeshafika lakini baadhi ya nyumba na taasisi hazikuwa zimeunganishwa. Endeleeni kuwa wabunifu ili kupeleka huduma bora kwa wananchi wengi zaidi,” amesema Mhe. Mgalu
Kamati hiyo pia imepongeza juhudi za Rais, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusukuma ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ambazo zimepelekea asilimia 23 ya wananchi kutumia nishati hiyo huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.
Katika hatua nyingine, Kamati imeisisitiza Wizara ya Nishati kuangalia namna bora ya kuziwezesha sekta binafsi ili mchango wake katika sekta ya nishati uongezeke zaidi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi, ikiwemo usambazaji wa nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema hali ya uzalishaji wa umeme nchini inaendelea kuimarika hadi kufikia megawati 4,437, huku lengo la Serikali ni kuzalisha megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 ambazo zitatokana na vyanzo mchanganyiko ikiwemo Jua na Upepo.
Akizungumzia upelekaji wa umeme kwenye maeneo ya uzalishaji, Mhe. Salome amesema Serikali inao mpango wa kupeleka umeme mkubwa katika kongani za viwanda ili kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza uzalishaji na kukuza Pato la Taifa.
Amebainisha pia kuwa, Serikali itakuja na mpango maalum wa kupeleka umeme katika maeneo ya migodi ili kuwezesha shughuli za uchimbaji kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Sambamba na hilo, ametoa wito kwa wakandarasi wa miradi ya umeme kuhakikisha taasisi za umma zinapewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme, zikiwemo shule, zahanati na visima vya maji, ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Vilevile, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini.