Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

YALIYOJIRI WAKATI WA HAFLA YA...

YALIYOJIRI WAKATI WA HAFLA YA UWEKAJI SAINI MAKUBALIANO YA AWALI YA MKATABA WA NCHI HODHI WA MRADI WA KUCHAKATA NA KUSINDIKA GESI ASILIA (LNG PROJECT)

*Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan*

#Huu ni mradi mkubwa na wa kimkakati kwa nchi yetu, tumekuwa na miradi mingine ya kimkakati kwa miaka ya hivi karibuni lakini yote ni sisi tunatoa mitaji na kutumia miradi lakini mradi huu una umahususi wake kwa sababu unaleta mtaji na unaleta mapato nchini.

#Maelekezo yangu ni kuendelea kusimamia maslahi ya nchi kwenye hatua zifuatazo za mazungumzo na pia ni muhimu kutambua kwamba katika majadiliano huwezi kukubaliwa kila unachokitaka hivyo nawasihi pande zote mbili muwe na uwezo wa kubadili mawazo kutokana na maongezi yatakayokuwepo.

#Mradi huu ni wa nchi nzima, lakini kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara lazima wayaone manufaa ya mradi huu, hivyo tusisahau mazingira mahususi ya Mikoa hii wakati wa majadiliano.

#Mchakato wa majadiliano, maandalizi na utekelezaji wa mradi lazima yapelekee kujenga uwezo wa Watanzania kwenye sekta hii, dhamira yetu ni kwamba katika miaka ijayo, vizazi vijavyo viweze kuvuna rasilimali za nchi kwa tija zaidi, manufaa zaidi na kwa kujitegemea zaidi.

#Lazima tuanze sasa kujenga uwezo wa Watanzania kushiriki kikamilifu na kutumia manufaa yatokanayo na mradi huu.

#Huu ni mradi mkubwa na lazima ulindwe, walindaji wakubwa ni sisi na sio Wawekezaji kwahiyo lazima tujitayarishe kwa hilo.

#Nataka TPDC liwe Shirika la kimkakati kwa nchi yetu ili kwa miaka ijayo shughuli zote mzifanye nyinyi kwa sababu katika mradi huu hatukuwa na Wataalam wa kutosha hadi tumetafuta msaada nje ya nchi.

#Wizara ya Fedha na Mipango pamoja Wizara ya Nishati nataka mkae mjadiliane ili kuona ni kwa namna gani ushiriki wa TPDC katika mradi huu unakuwa wa tija na manufaa makubwa zaidi.

#Mradi huu ni Watanzania wote hivyo nawaomba muanze kujipanga kwa sababu mradi huu mbali na mtambo wa kuchakata gesi na shughuli zake, kutakuwa na eneo maalum la kiuchumi litakalotoa huduma katika mradi.

#Sekta binafsi za Tanzania zianze kujipanga kuchukua nafasi za kutoa huduma kwenye mradi huo na wananchi pia ili tukuze uchumi wetu ndani kuliko kuwaachia watu wa nje waje watoe huduma na mapato yaende kwao.

#Ni mategemeo yetu kwamba Tanzania pia itapata maendeleo na ustawi wa watu wake kupitia uzalishaji wa gesi asilia kama ilivyo kwa nchi zenye miradi hii.

#Natumaini Kampuni za Kimataifa zitatilia maanani masuala haya katika majadiliano yanayoendelea ili kuhakikisha kuwa Taifa la Tanzania linaingia vyema kwenye ramani ya Dunia ya wazalishaji gesi na mazao yatokanayo na gesi.

#Nahimiza Wizara na kampuni inazoshirikiana nazo kuongeza kasi ya kutafuta gesi katika maeneo mengi nchini hasa kwa sababu gesi yetu ina sifa zote ambazo Wawekezaji wanazihitaji.

#Uwekezaji katika mradi huu unatarajiwa kugharimu takriban Shilingi trilioni 70, kwa mujibu wa tafiti, asilimia 10 ya kiasi hiki hutumika ndani ya nchi katika kipindi ambacho mradi unajengwa.

#Fedha hizi zitatumika katika ununuzi wa vifaa na kutoa huduma za ndani ya nchi ikiwemo huduma za usafirishaji, ukodishaji wa mitambo, chakula, ulinzi, bima na malazi.

#Serikali imejipanga kutoa kipaumbele maalum kwa Wakandarasi na watoa huduma wa ndani katika miradi hii, nazitaka sekta zote zitakazoguswa na mradi huu kwenda kukaa kujadili kwa pamoja ili kuanza kujipanga mradi unaendaje kiujumla.

*Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba*

#Hadi kufikia mwezi Mei, 2022, jumla ya futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia ziligunduliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

#Kati ya hizo, jumla ya futi za ujazo trilioni 47.13 ni katika vitalu vilivyopo katika kina cha bahari na futi za ujazo trilioni 10.41 ni katika maeneo ya nchi kavu, ugunduzi wa kiasi hiki kikubwa cha gesi asilia ulifanyika kwa ushirikiano wa Serikali na Makampuni.

#Utekelezaji wa mradi huu katika Mkoa wa Lindi utafanyika sambamba na uendelezaji wa miundombinu kwenye mkondo wa juu ili kuwezesha kuvuna rasilimali hiyo.

#Mradi huu mkubwa utabadilisha sura na taswira ya uchumi wa nchi yetu.

#Eneo ambalo mtambo utajengwa tayari limeshajulikana na kuwekwa katika miliki ya Serikali kwa kuwalipa fidia ya takriban Shilingi bilioni 5.71 wananchi 642 waliokuwa wakazi wa maeneo hayo.

#Baadhi ya manufaa ya mradi hii ni kuchochea ukuaji wa uchumi, kuiongezea Serikali Mapato, kuongeza ajira na kuongeza uwezo wa Watanzania kitaaluma.

#Kati ya miaka minne hadi sita ya ujenzi wa mradi huu kunatarajiwa kuwa na ajira 10,000 na baada ya kukamilika kwa ujenzi, ajira za kudumu zitakuwa 500.

#Wizara tumejipanga kuhakikisha Watanzania wanashiriki kwa ufanisi zaidi na tumejipanga kujenga uwezo wa rasilimali watu kuweza kuhudumia mradi, kushiriki na kupata manufaa kutoka kwenye mradi.

#Kwa maelekezo yako, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tumeamua kujenga chuo kikubwa cha ufundi Mkoani Lindi mahususi kwa ajili ya mafuta, gesi na umeme kama sehemu ya kujenga uwezo wa Watanzania na kutoa nguvu kazi katika mradi huu.

*Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,Mhandisi Felchesmi Mramba*

#Leo tutashuhudia Uwekaji wa saini wa makubaliano ya awali ya mkataba wa nchi hodhi baina ya Serikali na Makampuni yaliyogundua gesi kwenye vitalu na namba 1, 4, 2 na katika kina cha bahari ya Hindi.

#Utiaji saini huu unaweka msingi mkuu wa kukamilisha majadiliano ya mkataba wa ‘Host Government Agreement’ na mikataba mingine ya utekelezaji wa mradi wa kuchakata gesi asilia ambapo tunatarajia mazungumzo hayo kuendelea hadi Disemba, 2022.

*Wawakilishi wa Makampuni ya Kimataifa ya Mafuta, Jared Kuehi, Makamu wa Rais na Meneja Mkazi wa Kampuni ya Shell na Unni Fjaer, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Equinor.*

#Tunatambua jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka kipaumbele katika mradi huu, tunashukuru kwa nafasi mliyotupa ya kufanya kazi na Waziri Makamba pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

#Nataka wote mfahamu kuwa tunajisikia fahari kuwa na mahusiano mazuri kati yetu pia tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kutoa mchango wao katika mradi huu.

#Tutafanya kila kitu tunachokiweza ili mradi huu uendelee.

*Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano kutoka Tanzania,Mhandisi Charles Sangweni*

#Mnamo mwaka 2010-2016, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni tano za mafuta za Kimataifa zilihusika katika utambuzi wa gesi asilia nchini.

#Kufuatia ugunduzi huo, Serikali ilifanya maamuzi ya kuendeleza gesi hiyo kwa kuibadili kutoka katika hali ya hewa na kwenda katika hali ya kimiminika ili iweze kusafirishwa kwa wingi na kwenda kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

#Lengo la mkataba huu ni kuweka mfumo wa kimkataba unaolenga mambo mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi na kibiashara, kufafanua wajibu wa Serikali na Wawekezaji na udhibiti wa mradi husika ili uweze kuleta tija kwa pande zote mbili.

#Mkataba huu huanisha matarajio ya Serikali kutokana na mradi kupitia kodi, ushuru, ushirikishwaji wa wananchi na fursa za ajira.

#Malengo ya majadiliano hayo ni kuhakikisha Serikali na watu wake wanapata mapato na faida stahiki huku tukihakikisha mradi unatekelezeka kiufanisi.

*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*