ZAIDI YA MAJIKO 14,000 YA NISHATI SAFI YASAMBAZWA IRINGA.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba amesema Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa njia mbalimbali ikiwemo usambazaji wa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku pamoja na majiko banifu huku Mkoa wa Iringa ukiwa tayari umepokea mitungi ya gesi 9,000 pamoja na majiko banifu zaidi ya 5,000 yaliyosambazwa kwa wananchi.
Ameyasema hayo leo Mei 24, 2026 wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia Afrika na duniani ambapo amewasihi wananchi wa Kilolo kumuunga mkono katika juhudi za utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi ya kupikia.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali za wananchi katika sekta ya nishati ili kuhakikisha huduma bora ya umeme inapatikana kwa wananchi ikiwemo wa Jimbo la Kilolo mkoani Iringa.
Kwa maeneo ya mijini yenye sura ya Vijiji amesema yataunganishiwa umeme kwa sh. 27,000 tu kama ilivyoahidiwa katika bajeti ya Wizara ya Nishati 2026/2027.
“Katika Kitongoji cha Mtitu wananchi waliunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 lakini baada ya mradi kukabidhiwa TANESCO gharama ilibadilika na kufikia shilingi 320,000. Niwahakikishie kuwa maeneo yote yenye sura ya vijijini hata kama yako mjini yataunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 katika maeneo yatakayobainishwa”. Amesema Mhe. Salome.