Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 42...

​ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 42 KUBORESHA UMEME TABORA – BYABATO

ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 42 KUBORESHA UMEME TABORA – BYABATO

Zaidi ya shilingi bilioni 42 zimetengwa na Serikali kwa ajili ya kuboresha kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Kiloleni, wilayani Tabora mjini, mkoani Tabora ili kuimarisha huduma ya umeme mkoani humo.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato tarehe 10 Julai, 2021 alipotembeleakituo cha kupozea na kusambazaumeme cha Kiloleni kilichopo Tabora mjini, mkoani Tabora.

Naibu Waziri Byabato alisema, Tabora ni mkoa wa kimkati wenye fursa nyingi za maendeleo ikiwemo migodi, kilimo na viwanda hivyo, unahitaji kuwa na umeme wa uhakika kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa kasi.

Aliongeza kuwa, umeme wa uhakika mkoani Tabora utawezesha uendeshaji wa treni ya kisasa (Standard Gauge) ambayo uzinduzi wa shughuli za ujenzi wake unatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Naibu Waziri Byabato alieleza kuwa, kituo cha kupozea na kusambazaumeme cha Kiloleni, kinachopokea umeme kutoka mkoa wa Shinyanga na kusambaza katika wilaya za Tabora, Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui kikiwa na megawati 24 kilianza kazi mwaka 1989 hivyo ni muhimu kukiboresha ili kiwe na umeme wa uhakika na kuwa fedha zilizotengwa zitapelekea kituo hicho kuwa na megawati 72.

Aidha, Naibu Waziri Byabato alibainisha kuwa, Kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Kiloleni ni miongoni mwa vituo 9 vinavyotarajiwa kuboreshwa mkoani Tabora ili kuwa na umeme wa uhakika.

Vilevile, Naibu Waziri Byabato aliagiza kutengenezwa kwa transfoma iliyoharibika ndani ya Mwezi Julai, 2021 ili kuongeza nguvu ya umeme kituoni Kiloleni licha ya kuwa kuna transfoma moja inayofanya kazi.

Aidha, Naibu Waziri Byabato alielea kuridhishwa kwake na utendaji wa Ofisi ya TANESCO mkoa wa Tabora na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na usahihi ili kufikia malengo ya Kitaifa katika sekta ya Nishati.