Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

RAIS SAMIA AFUNGA NJIA YA KUCH...

RAIS SAMIA AFUNGA NJIA YA KUCHEPUSHA MAJI NA KUANZA UJAZAJI WA MAJI BWAWA LA JNHPP

RAIS SAMIA AFUNGA NJIA YA KUCHEPUSHA MAJI NA KUANZA UJAZAJI WA MAJI BWAWA LA JNHPP

ALIYOSEMA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

#Hili ni tukio muhimu la kihistoria na faraja nchini kwetu katika safari ya kukamilisha mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere hatua kwa hatua, hii inatoa ujumbe duniani kuwa Tanzania inaweza kutekeleza mambo makubwa ya kuweza kubadilisha taswira ya nchi na ulimwengu pamoja na kuweka alama mpya katika ramani ya dunia.

#Mradi huu utatuletea umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo endelevu na kutimiza ndoto iliyokuwepo tangu tumepata Uhuru, tunawashukuru wote walioshiriki kuleta fikra hii na walioshiriki katika utekelezaji wake.

#Nawapongeza sana Wizara ya Nishati, TANESCO, Katibu Mkuu Kiongozi, kampuni, benki, TANAPA, TAWA, TFS, TANROADS, vyombo vya Ulinzi na Usalama, wadau wote wa maendeleo pamoja na wote wanaosaidiana nao kwa kazi nzuri ya usimamizi na utekelezaji inayoendelea kufanywa.

#Ujenzi wa Bwawa la Nyerere ni kazi kubwa yenye ubora na viwango vinavyotakiwa, safari ya ujenzi ilianza kipindi cha Mwalimu Nyerere na katika kipindi cha Awamu ya Tano cha Hayati John Pombe Magufuli ujenzi ulianza kutekelezwa, pamoja na mikiki mikiki iliyokuwepo kuhusu suala hili lakini kazi ilianza na kupelekea matunda tunayoyaona hivi leo.

#Naishukuru sana Serikali ya Misri kwa kuwa pamoja nasi, salaam zimfikie Rais wa Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi kwa ushirikiano mkubwa anaotupa kwa kuhakikisha mradi huu unatekelezwa ipasavyo.

#Wakati napewa jukumu la kuongoza nchi hii mradi huu ulikuwa asilimia 37%, na leo namshukuru Mungu kuona umefikia 78.68%, natoa ahadi kwenu ndugu Watanzania kuwa nitausimamia mradi huu hadi ukamilike kama ulivyopangwa.

#Kama tulivyojuzwa hapo awali, hadi sasa kazi imekamilika kwa asilimia 78.68%, kinachoendelea hivi sasa ni kufunga mitambo ya kufua umeme na vifaa vingine kabla hatujaenda kwenye majaribio ya kuiwasha.

#Mradi huu ni mojawapo ya miradi mikubwa barani Afrika, Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia uwekezaji huu wenye faida nyingi zikiwemo za kuweka akiba kubwa ya maji na kuzalisha umeme hata kama mvua imepungua na kusaidia kudhibiti mafuriko ya mara kwa mara ya mto Rufiji.

#Mradi pia utasaidia katika kilimo cha uhakika cha umwagiliaji, utaimarisha na kufungua fursa nyingi za utalii katika eneo la Kusini mwa Tanzania hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na hivyo kutoa ajira za moja kwa moja na nyinginezo.

#Kupitia Bwawa hili, tumejenga daraja kubwa na bora kuiunganisha mikoa ya Kusini, kilichobakia ni barabara ambapo nawaelekeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (TANROADS) kuandaa mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Chalinze hadi Utete kupitia kwenye daraja hili, lengo ni kwamba watu wanaotoka Mtwara na Lindi kwenda Dodoma, Iringa au Arusha hatakuwa na haja ya kupitia Dar es Salaam hivyo njia hii itafupisha sana safari hizo.

#Naielekeza Wizara ya Uvuvi na Mifugo kuja na mipango mkakati ya ufugaji wa kisasa wa samaki ili tukuze uchumi wa watu wetu wa maeneo haya.

#Naielekeza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Aridhi, TAMISEMI na mamlaka nyinginezo mkapime maeneo hayo kwa kuyaweka kwenye mashamba makubwa kwa ajili ya kufanya mnada wa uwazi kwa wawekezaji wa uhakika katika kilimo, pia kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo yatakayokuwa na miundombinu ya umwagiliaji.

#Manufaa ya bwawa hili katika nyanja zote yatawezekana kama tutatunza mazingira katika vyanzo na mabonde ya mito inayoleta maji hapa bwawani, tutunze mazingira maana huu mradi tumeujenga kwa gharama kubwa na kujinyima vitu vingi muhimu, hivyo tuutunze kufa na kupona.

#Maji yanayopita hapa ni mengi sana, yanaweza kisaidia mahitaji ya maji safi na salama kwa mkoa wa Dar es Salaam na viunga vyake, namwelekeza Waziri wa Maji kwamba DAWASA iangalie namna ya kuyatumia maji haya na ujenzi wa bwawa hili utoe fursa ya kuanza mipango ya ujenzi wa kituo cha kupokelea maji katika eneo la Mloka ili maji hayo yaanze kutumika Dar es Salaam.

#Hakuna mkubwa mbele ya sheria, Wakuu wa Mikoa na Wilaya fanyeni kazi yenu bwawa hili lilindwe ipasavyo. Mto Ruaha Mkuu utachangia maji kwenye bwawa hili kwa 15%, Mto Kilombero utachangia 65%, Mto Luega utachangia 19%, hivyo watu wa maeneo hayo watunze mazingira ili kujaza bwawa la Nyerere.

#Wananchi, wafanyabiashara na taasisi zote ambazo zinachepusha maji katika bonde la mto Rufiji wazuiwe

#Siku chache zijazo tunasherehekea Siku Kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, nawatakia Wananchi wote heri nyingi na kuwaomba kuwa waangalifu ili tuwe na furaha.

ALIYOSEMA SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. DKT. TULIA ACKSON

#Leo inatengenezwa historia ya kuondoa tatizo la umeme nchini, hii ni suluhu ya kudumu. Niseme tu Rais Samia umefanya, unafanya na kuzidi, hivyo nakupongeza sana.

#Utekelezaji wa mradi huu haugusi tu kwenye eneo la kuleta suluhu ya kudumu kwa upatikanaji wa uhakika wa umeme lakini pia unagusa kwenye sekta nyingine muhimu ya upatikanaji wa uhakika wa maji kwa mikoa iliyopo karibu na bwawa hili.

#Kwa wingi wa maji haya, tunaamini tutakuwa na uhakika wa kupata chakula cha kutosha cha kulisha Taifa letu na dunia nzima kwani maji yatawasaidia wakulima kumwagilia mazao yao kwa uhakika.

*ALIYOSEMA WAZIRI WA NISHATI, MHE. JANUARY MAKAMBA*

#Nakushukuru Rais Samia kwa uongozi wako madhubuti katika nchi yetu kwani ushahidi wa uongozi wako, matokeo ya ustawi wa Watanzania unaonekana, pia amani, utulivu, umoja, upendo na mapatano vinaendelea kushamiri nchini.

#Kwa mujibu wa mkataba, pale fedha zinapochelewa kulipwa kwa kila hatua huwa kuna adhabu, hatujawahi kuchelewa hata mara moja kufanya malipo ya mradi huu na hadi leo hii hatudaiwi fedha yoyote.

#Rais Samia ulipoingia madarakani mradi huu ulikuwa umefikia 37%, katika kipindi cha miezi 20 ya uongozi wako, mradi huu umefikia 78%, tunakushukuru kwa kuusukuma kwa kasi mradi huu.

*ALIYOSEMA WAZIRI WA MAJI, NISHATI NA MADINI - ZANZIBAR, MHE. SHAIBU HASSAN KADUARA*

#Na sisi ni sehemu ya watu tutakaonufaika na uzalishaji wa umeme huu, hivi karibuni tuliondoa changamoto ya muungano ambapo tumekubaliana kuuziana umeme kwa bei nafuu ya Shilingi 130 kwa Uniti moja.

#Tunaendelea kukushukuru na kukupongeza kwa kusimamia kwa dhati muungano wetu, tunawapongeza pia TANESCO kwa ushirikiano mkubwa na Shirika letu la Umeme la ZECO.

*ALIYOSEMA MKURUGENZI MTENDAJI WA SHIRIKA LA UMEME TANZANIA (TANESCO), MAHARAGE CHANDE*

#Njia ya kwanza ya mradi huu ilikuwa ni njia ya kuchepusha maji ya mto, ujenzi wa njia ya mchepusho wa maji umefikia 97.97% na 3.2% iliyobaki kumalizika ni kazi ya kufunga lango kuu ya njia ya mchepusho wa maji itakayofanyika leo.

#Njia ya kuchepusha maji ina urefu wa mita 703 na upana wa kipenyo cha mita 12, kwa upande wa ujenzi wa tuta kuu umefikia 89.51% huku 10.5% zilizobaki ni kumalizia mageti ili bwawa linapojaa mageti yafunguliwe maji yaweze kutoka.

#Ukuta una uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni 32, maji haya ni mengi zaidi ya maji yanayopatika ziwa Rukwa yakishajaa katika tuta. Huku maji yanayopita katika njia moja ya mashine ni takriban lita 225,000 kwa sekunde.

#Usimikaji na ufungaji mitambo kwenye jengo la kufulia umeme umefikia 60.46%, ujenzi wa kituo cha kupokea na kusafirisha umeme umefikia 97.20%.

#Ujenzi wa njia ya kupitisha umeme umefikia 80%, ujenzi wa daraja litakalounganisha mikoa ya kusini na kaskazini umefikia 96.87% na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi umefikia 84.89%.

#Mradi huu unakadiriwa kutumia Shilingi trilioni 6.5 ambazo ni fedha zetu zinazotokana na kodi za Watanzania ambapo mpaka kufikia Novemba, Serikali imemlipa Mkandarasi Shilingi trilioni 4.5 sawa na 70% za mradi.

#Hadi kufikia mwezi Novemba, 2022, mradi huu umeajiri watu 12,275 ambapo kati ya walioajiriwa, Watanzania ni 11,164 sawa na 90.97%.

#Mradi huu umejengwa kwa kuzingatia mazingira kama miradi mingine ili usilete athari za mazingira. Ukuta uliojengwa kwenye mradi huu una matundu ambayo yatapitisha maji kidogo ili kuhakikisha viumbe na maisha nyuma ya ukuta yanaendelea.

*ALIYOSEMA MKUU WA MKOA WA PWANI, MHE. ABUBAKAR KUNENGE*

#Nishati ni muhimu sana kwa mkoa huu kwani ni mkoa wa uwekezaji na biashara, mkoa wa viwanda na kilimo, yote haya yanahitaji zaidi nishati ya umeme, maji na barabara n.k

#Bwawa hili lina fursa nyingi, sisi wakazi wa Pwani tumejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama wa eneo hili unakuwa ni kipaumbele chetu pia tutalinda mazingira pamoja na vyanzo vya maji.

*ALIYOSEMA MKUU WA MKOA WA MOROGORO, MHE. FATMA MWASSA*

#Nawakaribisha wote mliojumuika hapa katika kuweka historia ya nchi yetu. Kipekee, tunakushukuru na kukupongeza Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza kutekeleza kwa kasi kubwa mradi huu mkubwa wa bwawa la Julius Nyerere mpaka kufikia hatua hii ambapo utafunga njia ya mchepusho wa maji ya bwawa hili.

#Mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere utakapokamilika, 93% ya umeme unaozalishwa nchini kote utakuwa unazalishwa Morogoro kupitia mabwawa ya Kihansi, Kidatu na JK Nyerere.

*ALIYOSEMA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA SERIKALI YA MISRI, MHE. SAMEH SHOUKRI*

#Naipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada kubwa ambazo imezifanya kwa kuthubutu kuanzisha mradi huu, kwa sasa umefikia 78%, tukio hili la ujazaji wa maji ni hatua kubwa katika kufanikisha mradi huu.

#Tanzania imewekeza jumla ya Dola za Marekani bilioni 2.9 kwa ajili ya kuzalisha umeme wa Megawati 2115, Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere utabaki kuwa ni moja ya mradi mkubwa wa kimaendeleo katika bara letu.

*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*