KAMATI MPYA YA UKAGUZI WIZARA YA NISHATI YAFANYA ZIARA KATIKA MIRADI YA UMEME MKOANI PWANI
Kamati mpya ya Ukaguzi ya Wizara ya Nishati imefanya ziara katika miradi ya umeme mkoani Pwani ili kujionea utekelezaji wa miradi hiyo hali itakayopelekea Kamati husika kumshauri vyema Katibu Mkuu Wizara ya Nishati juu ya usimamizi wa rasilimali za Wizara ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi.
Ziara hiyo imefanyika katika Mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Chalinze mkoani Pwani tarehe 19 na 20 Mei 2025
Baada ya kujionea utekelezaji wa miradi hiyo ambayo imekamilika, Mwenyekiti wa Kamati, Mhandisi Kenneth Nindie ameipongeza Serikali kwa kazi Kubwa inayofanya kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza fedha nyingi katika miradi ya umeme, hivyo Wizara ya Nishati wajibu wake ni kufanya usimamizi mzuri wa miradi ili thamani ya fedha ionekane.
Kamati hiyo pia imewataka wakandarasi wanaopewa kazi ya kutekeleza miradi kuwa wazalendo kwa kuzingatia viwango na ubora ili miradi inayofanyika idumu kwa muda mrefu na kuleta matokeo chanya kwa Watanzania.
"Tunaipongeza Serikali kwa kweli inafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi mikubwa katika nchi yetu kwa manufaa mapana ya wananchi, kikubwa tunawasihi wakandarasi kuwa wazalendo katika kutekeleza majukumu yao, mikataba iliyowekwa izingatiwe kwa kutekeleza kazi kwa viwango na Ubora ili miradi hii iwe na tija kwa Taifa." Amesema Nindie