Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

AFRIKA TUNAYAPA KIPAUMBLE MATU...

AFRIKA TUNAYAPA KIPAUMBLE MATUMIZI YA NISHATI SAFI ILI KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI-DKT. BITEKO

Asema Sera na Sheria zinazowekwa zinahimiza matumizi ya Nishati Safi


Afungua Mkutano wa Awali EAPCE'25

Ataka utumike kujadili na kuweka mipango itakayowezesha matumizi ya
Nishati Safi

Ataka mkazo kuwekwa kwenye Nishati Safi ya Kupikia kwani matumizi ya
kuni na mkaa bado ni makubwa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema
licha Bara la Afrika kuwa na mchango mdogo katika uchafuzi wa hali ya
hewa, nchi za Afrika bado zimekuwa mstari wa mbele katika kuendesha
ajenda ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuijumuisha katika mifumo yao ya
kisheria na udhibiti ikiwemo ya kuhakikisha kuwa nchi zinahama kutoka
kwenye matumizi ya nishati chafu na kutumia nishati safi ili kuiepusha
dunia na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 4 Machi, 2025 jijini Dar es Salaam
wakati akifungua Mkutano wa awali kuelekea Kongamano na Maonesho ya
Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25)
litakaloanza rasmi kesho ambapo mkutano huo wa awali ulilenga kujadili
mipango na mikakati itakayopelekea matumizi ya nishati safi katika
maeneo mbalimbali ikiwemo kupikia na vyombo vya usafiri (CNG).

Amesema mkutano wa EAPCE’ 25 ni jukwaa muhimu kwa nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki na wadau wengine kujadili mipango na
mikakati kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi hasa ikizingatiwa
kwa sasa dunia inapambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambazo
kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na shughuli za binadamu huku tafiti za
kisayansi zikionesha kuwa viwango vya utoaji wa hewa ya ukaa
vimeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya
Viwanda.

“ Nataka nichukue nafasi hii kuwaomba wote muutumie mkutano huu
kujadili masuala ambayo yatatufanya sisi wana Afrika Mashariki, tuweze
kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyokuwa safi kwenda kwenye
matumizi ya nishati iliyosafi, lazima mtambue kwamba mkutano huu wa
awali haujatokea kwa bahati mbaya, kama jamii tunayo kazi ya kufanya
ya kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi kwenda matumizi ya
nishati safi.” Amesisitiza Dkt.Biteko

Ameeleza kuwa, sheria nyingi zinazopitishwa kwa sasa barani Afrika
zinahimiza uchumi wa kijani, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuwa
na maendeleo endelevu ambapo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa
upande wake imeandaa Sera ya Mabadiliko ya Tabianchi ikiwa ni
uthibitisho wa dhamira ya kanda hiyo katika kushughulikia tatizo la
mabadiliko ya tabia nchi na kuhimiza matumizi ya nishati safi.

Ametaja baadhi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kuwa ni pamoja na
ukame mkali, mafuriko, kupotea kwa viumbe hai, kupungua kwa vyanzo
vya maji safi, kuyeyuka kwa barafu, na ongezeko la magonjwa
yanayohusiana na tabianchi kama vile saratani ya ngozi.

Dkt.Biteko ameeleza kuwa suala la mabadiliko ya tabia nchi linatiliwa
mkazo pia katika ngazi ya dunia na hii imepelekea kuwepo kwa mikataba
mbalimbali ya kimataifa ukiwemo wa Kyoto, Montreal na Paris ambapo
nchi zilizoendelea na zinazoendelea zinaandaa na kutekeleza mikakati
inayohusiana na tabianchi ikiwemo kujikita katika matumizi ya nishati
safi zisizochafua mazingira ikiwemo Gesi Asilia.

Kuhusu upatikanaji umeme amesema Afrika ndiyo Bara linalokabiliwa na
upungufu mkubwa wa nishati duniani, ambapo asilimia 75 ya watu
wanaokosa nishati duniani wanapatikana barani humo lakini juhudi
zinafanyika ili kuwezesha upatikanaji wa nishati na hili
lilithibitishwa kupitia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu
Nishati uliofanyika Tanzania Januari mwaka huu ambao uliweka mikakati
ya kuongeza upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo
mwaka 2030 ambayo ni hatua muhimu kuelekea mabadiliko ya kinishati.

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia amesema mabadiliko yanahitajika ili
kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi kwani idadi kubwa ya watu
barani Afrika bado wanategemea kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia
akitolea mfano nchini Tanzania, takriban asilimia 81 ya kaya
zinatumia kuni na mkaa kama vyanzo vyao vikuu vya nishati ya kupikia,
hali inayosababisha upotevu wa misitu wa takriban hekta 469,420 kila
mwaka akitanabaisha kuwa mwelekeo huo wa kutisha unahitaji hatua za
haraka na za pamoja ili kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia
barani kote.

Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo nchini Tanzania, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,
ambaye ni kinara wa ajenda nishati safi ya kupikia kitaifa na
kimataifa kwa ujumla amechukua hatua madhubuti kwa kutekeleza Mkakati
wa Kitaifa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) ambao unalenga
kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya
kupikia ifikapo mwaka 2034.

Aidha amesema kuwa, matumizi ya gesi asilia kama nishati ya kuendeshea
vyombo vya usafiri pia ni muhimu katika kuelekea kwenye matumizi ya
nishati safi akieleza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha
mazingira kwa wawekezaji binafsi kushiriki katika ujenzi wa Vituo vya
Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) na kuboresha sera na mifumo ya
udhibiti.

Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga kwa upande wake amesema
mkutano huo wa awali unaweka msingi wa Kongamano la 11 la Mafuta kwa
Nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki litakaloanza kesho Machi 05, 2025.

"Siku ya leo kutakuwa na mada mbalimbali zitakazozungumzwa, ambazo
zitakuwa na majadiliano yatakayoweka msingi kwa ajili ya mkutano mkuu
utakaoanza kesho na kufanyika kwa siku tatu, mkutano huu ni muhimu
katika kuwaweka wadau pamoja na kujadiliana masuala ya msingi ambayo
yatazisaidia Nchi za jumuia ya Afrika Mashariki katika Sekta ya Mafuta
na Gesi.” Amesema Kapinga

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba
amesema kuwa mkutano huo wa Mafuta na Gesi unaenda sambamba na
Maonesho ya bidhaa za mafuta na gesi pamoja na kazi mbalimbali
zinazofanyika katika sekta miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.

Ameeleza kuwa, Mkutano umelenga kuangalia namna bora ya kuhama kutoka
kwenye nishati zinazochafua mazingira kwenda kwenye nishati safi
zisizochafua mazingira ikiwa ni kampeni ya dunia ambayo imetokana na
malengo ya dunia ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2050 hadi 2060
dunia iwe imeweza kuhamia kwenye nishati safi kwa kiasi kikubwa.

Mhandisi Mramba ameeleza kuwa, katika mkutano huo nchi zitapata
nafasi ya kuelezea maendeleo waliyofanya katika eneo la mafuta na gesi
ambapo Makatibu Wakuu na Mawaziri watazungumza kuhusu mafanikio,
mipango na kazi zilizofanyika tangu kufanyika kwa mkutano uliopita wa
EAPCE.

Amesema katika mkutano wa EAPCE’25 wataalam, watafiti na wabunifu
mbalimbali watazungumzia ugunduzi wa mafuta na gesi, sehemu ambazo
vitalu vinanadiwa na kukaribisha uwekezaji kwa nchi za EAC.