BAHI ENGLISH MEDIUM YA ACHANA NA MATUMIZI YA KUNI.
Shule ya Mchepuo wa Kingereza ya Bahi imeanza kunufaika na matumizi ya nishati safi ya kupikia baada ya kuachana na matumizi ya kuni, hatua iliyosaidia kupunguza gharama za nishati na kurahisisha shughuli za upishi shuleni.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi. Farida Ngolo, amesema hapo awali shule hiyo ilikuwa ikitumia kuni kwa ajili ya kupikia, hali iliyosababisha gharama kubwa za upatikanaji wa nishati na kuongeza mzigo wa uendeshaji wa shughuli za shule.
Amesema tangu shule hiyo ianze kutumia nishati safi ya kupikia, imepata nafuu kutokana na kupungua kwa gharama za nishati, huku shughuli za maandalizi ya chakula zikiendelea kwa ufanisi zaidi.
“Mfumo huu umetusaidia kwa kiasi kikubwa hapo awali tulikuwa tunatumia gharama kubwa katika upatikanaji wa nishati ya kupikia, lakini sasa tumepata nafuu na shughuli zetu zinaendelea kwa ufanisi zaidi,” amesema Bi. Farida Ngolo.
Aidha, Bi. Farida Ngolo amesema shule hiyo imepokea majiko manne pamoja na sufuria zake kupitia mpango huo, na imeahidi kutunza vifaa hivyo pamoja na miundombinu yake ili viendelee kutumika kwa muda mrefu na kutoa manufaa kwa shule na wanafunzi.
Vilevile, ameishukuru Serikali pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kwa kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia shuleni hapo.
Kwa upande wake, Mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati, Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Bw. Deo Alex, ameipongeza shule hiyo kwa kuachana na matumizi ya kuni na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia, kwani hatua hiyo itasaidia kulinda mazingira.
Bw. Deo amesisitiza umuhimu wa shule hiyo kuendelea kutunza majiko na miundombinu iliyotolewa ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kuendelea kunufaisha shule pamoja na wanafunzi.
Hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, kwa lengo la kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kupunguza gharama za uendeshaji, kulinda afya za watumiaji na kuhifadhi mazingira.